BODI mpya ya kupanga mishahara kwa sekta binafsi inatarajiwa kuanza kazi wakati wowote kuanzia Agosti mwaka huu, baada ya bejeti kuu ya serikali kupita.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Nicholas Mgaya alisema, bodi hiyo itakuwa na wajumbe 20 wakijumuisha wanne kutoka kila eneo.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni wawakilishi kutoka serikalini, chama cha waajiri, vyama vya wafanyakazi na wataalamu.
“Kila eneo litatoa wawakilishi wanne na sisi wafanyakazi tayari tumeshapendekeza majina yetu na maeneo mengine nayo yamekwisha pendekeza majina”.
Alisema, kinachosubiriwa ni Waziri anayehusika na Utumishi (Angella Kairuki) kutangaza kwenye gazeti la Serikali ili bodi hiyo ianze kazi Agosti, mwaka huu.
Bodi hiyo inaundwa baada ya serikali kufuta bodi za kupanga mishahara za kisekta ambazo zilionekana kutumia fedha nyingi kuziendesha.
Bodi hizo kwa mwaka jana zilitumia Sh mil 450 kuziendesha.
“Hili wazo la kuundwa kwa bodi mbili tu yaani ya sekta binafsi itakayojumuisha sekta 12 za binafsi na bodi ya kupanga mishahara ya sekta ya umma ilitolewa na serikali nasi wafanyakazi tukakubaliana nalo. Sasa hivi kilichobaki ni kuundwa kwa bodi ya kupanga mishahara ya utumishi wa umma,” alisema.
Alisema licha ya kutofahamu kima kipya cha chini ya mshahara kwa watumishi wa serikali ambacho kinatarajiwa kutangazwa wakati waziri anayeshughulikia utumishi atakapotangaza, Tucta wanasisitiza kupata kima cha chini sekta zote kiwe Sh 750,000 bila kukatwa kodi.
chanzo;habarileo.
Comments