Askari wa UN: Tutaendelea kusimamia amani nchini Mali.

Mkuu wa kikosi cha askari wa Umoja wa Mataifa wa kusimamia amani nchini Mali, amesisitizia azma ya askari hao ya kuendeleza operesheni za kudumisha usalama na amani nchini humo.

Koen Davidse aliyasema hayo jana katika kikao cha 29 cha uratibu wa wakuu wa askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa eneo la magharibi mwa Afrika huko mjini Dakar, Senegal na kusisitizia azma ya kuendelezwa mazungumzo na makundi husika nchini Mali kuhusiana na suala la amani na kutekelezwa makubaliano ya amani nchini humo. 

Davidse amesema kuwa kutatuliwa mgogoro wa Mali kunahitajia ushirikiano wa askari wa Ufaransa wanaotekeleza operesheni zinazoitwa Barkhane, askari wa Umoja wa Mataifa na wanamgambo wa nchi hiyo. 

Ameongeza kuwa, hivi sasa askari hao wa UN wako katika hatua ya kuboresha hali ya mambo nchini humo na kwamba kuharakishwa mwenendo wa kutekelezwa makubaliano ya amani kwa ajili ya kurejeshwa usalama, ndilo jambo linalopewa kipaumbele. 

Kadhalika Koen Davidse amelaani vikali shambulizi la siku ya Jumatano dhidi ya askari wa Umoja wa Mataifa nchini Mali ambalo lilipelekea askari watano kuuawa na wengine watatu kujeruhiwa.
chanzo;parstoday.

Comments