SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, amewataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kufanya kazi kwa kujituma kwa ajili ya kuwatumikia wananchi licha ya kwamba wajumbe wengi wanaounda baraza hilo wanatoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kazi na majukumu makubwa yanayowakabili wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni kuwatumikia wananchi katika majimbo ya uchaguzi, bila ya kujali itikadi za vyama vya siasa kwani maendeleo hayachagui chama wala itikadi.
Maulid alisema matarajio makubwa ya wananchi walio wengi ni kuona wawakilishi wao wanafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Serikali iliyopo madarakani kwa ajili ya kuleta maendeleo na kupambana na umasikini.
“Hayo ndiyo matarajio ya wananchi walio wengi kuona kwamba wajumbe wao wa Baraza la Wawakilishi wanafanya kazi kubwa ya kuleta na kuharakisha maendeleo bila ya kubaguana kwa misingi ya itikadi za kisiasa, kwani kwa kawaida maendeleo hayachaguwi chama wala hayana itikadi za kisiasa,” alisema.
Aliwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM kufanya kazi kwa juhudi zote ikiwemo kuibana Serikali ili itoe ufafanuzi wa mambo mbali mbali ya msingi kwa maendeleo ya wananchi, kwani huo ndiyo wajibu wao kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.
Alisema huo ndiyo wajibu na majukumu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhoji matumizi ya fedha za Serikali ambazo huitishwa katika bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha kwa ajili ya kuidhinishwa kwa matumizi.
“Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi miongoni mwa majukumu yenu ni hayo, kuhoji matumizi ya fedha za Serikali kwa ajili ya maendeleo pamoja na kupitisha bajeti ya Serikalikwa mwaka wa fedha ili yaidhinishwe kuanza matumizi yake,” alisema Maulid.
chanzo;habarileo.
Comments