Wapinzani wataka Rais wa Afrika Kusini ajiuzulu.

Wapinzani wa serikali ya Afrika Kusini wametaka Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo ajiuzulu
Chama kikuu cha upinzani bunge jana (Ijumaa) kilitaka kuchukuliwe hatua zote za lazima nje ya bunge; za kumlazimisha Rais Jacob Zuma kujiuzulu kama bunge la nchi hiyo litashindwa kufanya hivyo.
Mmusi Aloysias Maimane, mkuu wa chama kikuu cha upinzani katika Bunge la Afrika Kusini cha Democratic Alliance (DA) amewaambia waandishi wa habari kuwa, Zuma anapaswa kuondolewa madarakani haraka iwezekanavyo.
Amesema, "leo hii hukumu ya Mahakama ya Katiba iko wazi." Ameongeza kuwa: "Rais Jacob Zuma amevunja vibaya katiba jambo ambalo limefunguwa uwanja wa kuitwa bungeni kujieleza. 
Ningelikuwa mimi, ningelianza mapema kuandika barua ya kujiuzulu."
Matamshi hayo yamekuja siku moja baada ya Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini kutoa hukumu dhidi ya Jacob Zuma inayosema kuwa, Rais huyo wa Afrika Kusini alikiuka miongozo ya katiba kwa kukataa kutii maagizo ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma kuhusiana na kuirejeshea serikali sehemu ya dola milioni 16 za Marekani zilizotumika kukarabati makazi yake binafsi.
Ikumbukwe kuwa, Jaji Mkuu wa Afrika Kusini, Mogoeng Mogoeng ameipa Wizara ya Fedha ya nchi hiyo siku 60 kuamua ni kiasi gani Zuma anapaswa kukirejesha serikalini na baada ya hapo Rais huyo atakuwa na siku 45 za kulipa fedha hizo. 
Mogoeng amesema ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Umma ni moja ya taasisi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kupiga vita ufisadi nchini humo.
chanzo;kiswahili.irib.ir

Comments