BUNGE la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, limetoa ufafanuzi kuhusu zabuni iliyotolewa na Jeshi la Polisi nchini kwa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd yenye thamani ya Sh bilioni 37, inayodaiwa kuwa na harufu ya ufisadi.
Mwaka 2011, Kampuni hiyo ilipewa zabuni ya kufunga mashine za alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini ambapo inadaiwa imeshalipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37, sawa na asilimia 99 ya malipo yote.
Hata hivyo, kampuni hiyo imedaiwa kuwa pamoja na kulipwa fedha karibu zote, yenyewe imefunga mashine katika vituo 14 pekee katika jiji la Dar es Salaam, ambavyo pia inadaiwa havijulikani maeneo vilipo.
Taarifa ya jana ya Bunge iliyotumwa kwa vyombo vya habari, imefafanua kuwa kumekuwa na upotoshaji kuhusu agizo la Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu zabuni hiyo.
“Kumekuwa na taarifa zinazoendelea kupotosha umma na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilipokuwa ikitekeleza majukumu yake Aprili 5, 2016 ililitaka Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba ulioingiwa Kati ya Jeshi hilo na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd.
“Ofisi ya Bunge inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili kwamba, taarifa hizo si za kweli na zina lengo la kupotosha umma kutokana na kile kilichoamuliwa na kamati hiyo,” ilieleza taarifa hiyo.
Ufafanuzi Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Bunge, wakati vyombo vya habari vinaeleza kuwa PAC imeagiza mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni hiyo, ukweli ni kwamba kamati hiyo, haijaagiza kupatiwa mkataba wa zabuni hiyo.
Badala yake taarifa hiyo imefafanua kuwa Kamati hiyo iliomba Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kuwasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa Ofisi ya Katibu wa Bunge, ili Kamati ichambue na kujadili maelezo hayo kabla ya kupendekeza kwa Bunge hatua zaidi za kuchukua.
Aidha, Ofisi ya Bunge kwa maelezo ya taarifa hiyo, ilimwandikia barua Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Ndani Aprili 12 mwaka huu, kumtaka kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maagizo ya PAC yaliyotokana na kikao hicho cha Aprili 5, 2016 kabla ya Aprili 18, 2016 kama ilivyoshauriwa na kamati.
“Ni vyema umma ukafahamu kuwa kilichoombwa na kamati ni maelezo ya utekelezaji wa mkataba huo na si mkataba kama inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari ambapo Ofisi ya Bunge iliomba maelezo hayo yawasilishwe kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016,” imefafanua taarifa hiyo.
chanzo;habarileo.
Comments