Uhakiki wa Watumishi hewa wazua Kizaazaa hospitali ya wilaya Temeke.


Hali ya sintofahamu iliikumba Hospitali ya Temeke jana asubuhi, baada ya wakaguzi kufika kwa ajili ya kufanya uhakiki wa watumishi hewa hospitalini hapo. 
Hali hiyo ilisababisha wagonjwa kuachwa solemba huku watumishi wakifuata vyeti nyumbani. 
Wakaguzi hao ambao waliwasili hospitalini hapo asubuhi, walisababisha kazi ya kuhudumia wagonjwa kulegalega baada ya watumishi wengi kuonekana kuhaha kunusuru ajira zao. 
Baadhi ya wagonjwa walilalamikia huduma mbovu iliyokuwa ikitolewa kwa sababu wengi wao walichukua muda mrefu kupata huduma kutokana na wauguzi na madaktari wengi kuondoka ghafla kazini. 
Mgonjwa, Monica Kessy aliyekuwa akisubiri huduma alisema daktari aliyekuwa akiwahudumia aliondoka ghafla bila kuwaaga hivyo kuwalazimu wagonjwa kupanga foleni kwa daktari mmoja aliyebakia. 
“Ilipofika saa tano hivi, tukaona manesi na madaktari wanatoka na kukaa vikundi wakizungumzia suala la uhakiki wa watumishi hewa, wengine wakaanza kuondoka baadaye tukasikia tangazo kuhusu uhakiki, watumishi wengi wengi wakaondoka,” alisema Monica. 
Mgonjwa mwingine, Ali Bakari (74) aliyekuwa akisubiri huduma katika dirisha la wazee alisema, “Nimefika na mjukuu wangu saa nne asubuhi, nimefanikiwa kupata kipimo kimoja kati ya viwili ninavyotakiwa kufanyiwa ili nipatiwe dawa, lakini wapimaji wameondoka ghafla nalazimika kuwasubiri.” 
Mmoja wa wauguzi ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema wafanyakazi wengi walikuwa hawana taarifa juu ya ukaguzi kwa siku ya jana. 
“Usipowasilisha vyeti utaonekana wewe mtumishi hewa, ili kuliepuka hilo kila mmoja anatetea ugali wake, masjala hatuwezi kutosha wote, wengine tukarudi nyumbani kuchukua vyeti, ndiyo narudi sasa,” alisema. 
Alipoulizwa kuhusu hali hiyo Mganga Mkuu wa Hospitali ya Temeke, Amani Malima alisema huduma zinaendelea na uhakiki unaendelea. 
“Huduma inaendelea haijasimama, watumishi walitangaziwa tangu juzi kwamba kutakuwa na uhakiki kwa mara nyingine, lakini inaonekana hawakujiandaa na kazi ya uhakiki inaendelee,” alisema Dk Amani. 
Alipoulizwa kuhusu kutoonekena kwa baadhi ya wauguzi na madaktari hospitalini hapo, alisema tangazo lilitoka tangu juzi. 
chanzo;darwaya.com.

Comments