Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoa wa Arusha imetahadharisha waandishi wa habari kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani watakaohusika hawataonewa haya.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Juventus Baitu alisema waandishi wa habari ni muhimu katika kusaidia utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Alisema ni vyema kila mwandishi akajitathmini, kwasababu tayari ana taarifa za baadhi yao kujihusisha na masuala ya rushwa na mkoa unawafuatilia.
“Hivyo nawasihi ndugu zangu hatutamwonea mtu haya wala kumwogopa mtu, ili mradi umehusika na rushwa tutakunasa tu, muhimu jiepushe na rushwa,” Baitu alisisitiza.
Alikataa kuwataja waandishi wanaotuhumiwa kuhusika na masuala ya rushwa, kwa sasa.
Aidha, Baitu alisema taasisi yake imedhibiti mianya ya rushwa katika ununuzi na usambazaji wa dawa unaofanywa na Halmashauri ya Jiji la Arusha, katika vituo vya afya na zahanati zake.
Baitu alisema katika ufuatiliaji wao wamebaini kuwa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara vinapelekwa idadi pungufu kulinganisha na taarifa zilizopo katika halmashauri ya Jiji hilo.
Aidha, alisema pia udhibiti huo wameufanya katika hospitali teule ya Selian iliyopo Halmashauri ya Arusha, ambako kulikuwa na mianya ya rushwa
katika matumizi ya mishahara kutoka serikalini kwenda hospitali hiyo.
Alitaja maeneo mengine waliyofanikiwa kudhibiti mianya ya rushwa kuwa ni kwenye ugawaji wa viwanja katika kijiji cha Oltepes Wilayani Longido, ambapo
walipofuatilia walibaini wananchi hawakushirikishwa katika hatua zote za mradi kuanzia kupima hadi ugawaji wa viwanja.
chanzo;ippmedia.
Comments