TAASISI ya Kiislamu ya HAIAT imeiomba Serikali kuweka kitivo cha lugha ya Kiarabu katika vyuo vikuu nchini ili kusaidia wanafunzi katika mawasiliano ndani na nje ya nchi.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Shehe Abdallah Ndauga wakati wa uzinduzi wa semina ya walimu wanaofundisha lugha ya Kiarabu kwa shule za awali, msingi na sekondari.
Ndauga alisema uwepo wa lugha hiyo vyuoni utasaidia wanafunzi kuelewa lugha hiyo ambayo wataitumia nchini pamoja na kuwasiliana na mataifa mbalimbali.
“Endapo lugha hii ya kiarabu ikienea nchini natumaini waumini wengi wa dini ya Kiislamu wataweza kusoma na kukielewa kitabu kitakatifu cha Kurani tofauti na ilivyo sasa wengi wao hawaielewi na kuishia kujua maneno machache,” alisema.
Alisema asilimia kubwa ya maandiko ya Kiislamu yanatumia lugha ya Kiarabu ambayo ikitumika nchini itawaunganisha waumini wa mataifa mbalimbali.
Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi alisema uwepo wa lugha hiyo nchini utawasaidia Watanzania wengi ambao wangetamani kuisoma na kuitumia katika mambo mbalimbali ikiwemo kusoma vitabu vya Kurani ambavyo baadhi ya waumini wa dini hiyo hawajui lugha hiyo, hivyo kusababisha kutoelewa kitabu hicho.
“Msiwe wale wanaojivisha mizigo katika vichwa vyao huku hawana maslahi na walichobeba hawajui maana yake, ninawashukuru sana hivi vikundi kuja kutufundisha lugha ya Kiarabu maana ilikuwa kilio changu cha muda mrefu hivyo naamini wengi wataielewa,” alisema Mwinyi.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo alisema kuna baadhi ya vyuo nchini vinafundisha lugha ya Kiarabu ikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro na Chuo Kikuu cha Zanzibar.
Alisema ili kufikia lengo serikali itahakikisha inaweka mazingira wezeshi kwa walimu watakaofundisha lugha hiyo ili watoe elimu hiyo kwa maslahi mapana ya nchi.
chanzo;habarileo.
Comments