SMZ yashauriwa kutafuta nishati mbadala.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imetakiwa kuendelea na utekelezaji wa mradi wa matumizi sahihi ya usimamizi endelevu wa ardhi na usajili, pamoja na kutafuta vyanzo vya nishati mbadala, kama njia ya kupiga hatua ya maendeleo.
Ushauri huo ulitolewa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Ramadhan Abdalla Shaaban, wakati akikabidhi ofisi kwa Waziri aliyeteuliwa na Rais, Salama Aboud Talib huko Vuga mjini Unguja.
Alisema, Zanzibar ikiwa ni kisiwa inatakiwa kuendelea na mikakati yake ya kutumia vizuri rasilimali ya ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali, ikiwemo kilimo, kwani baadaye ardhi huweza kwisha huku mahitaji ya binadamu yakiongezeka.
Alisema, matukio ya uvamizi wa ardhi kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa makazi ya kudumu bila ya kusajiliwa ni tatizo kubwa lililosababisha ekari tatu zilizogawiwa na Serikali kwa kazi za kilimo kutumiwa kwa ujenzi wa nyumba za kuishi.
“Njia pekee ya kuwa na matumizi sahihi ya ardhi kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo ujenzi na kazi za kilimo ni kuendelea na mradi wa usajili wa ardhi ambao ndio mkombozi katika kuinusuru ardhi iliyopo sasa kuvamiwa kwa kazi ambazo hazina tija,” alisema.
Aidha, Shaaban alisema katika kipindi cha miaka mitano Serikali imekuwa ikifanya utafiti kwa ajili ya kuwezesha Zanzibar kuwa na nishati mbadala na kujitegemea kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa na kuachana na chanzo kimoja cha umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Akizungumza katika makabidhiano ya ofisi,Waziri Salama Aboud Talib alikiri kuwa wizara inakabiliwa na changamoto kubwa inayotokana na ukuaji wa idadi ya watu, pamoja na matumizi ya ardhi ndogo iliyopo kwa maendeleo ya taifa na binadamu kwa ujumla.
Alisema, miongoni mwa mambo yatakayopewa kipaumbele ni usajili wa ardhi na matumizi sahihi kwani kumejitokeza tatizo la uvamizi wa ardhi kwa ajili ya ujenzi hata katika vyanzo vya maji safi na salama. SMZ imeanzisha msako dhidi ya watu waliouza hekari tatu walizopewa kwa ajili ya matumizi ya kilimo.
Ardhi hiyo ilitolewa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Hayati Abeid Amaan Karume, kutokana na kutaifishwa kwa ardhi mara baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964 .
Inadaiwa badala ya kutumia maeneo hayo kwa kilimo, yamegeuzwa viwanja na kuanzisha ujenzi wa nyumba za kudumu za makazi kinyume na sheria ya umiliki wa eka hizo.
Zaidi ya watu 10 wamefutiwa umiliki wa eka tatu zilizotolewa na Serikali baada ya kubainika kuziuza na kugawiwa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za kudumu za kuishi wananchi katika maeneo ya mkoa wa Mjini Magharibi na Kati Unguja. Maeneo ambayo ardhi imekuwa ikiuzwa kiholela ni Mwera, Kiyanga pamoja na Mwanakwerekwe.
chanzo;habarileo.

Comments