MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameyataka makampuni yanayowekeza nchini kufuata misingi ya kisheria ya uwekezaji ili kusiwe na changamoto katika kipindi chote cha kutekeleza miradi hadi kukamilika.
Aliyasema hayo jana kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa ‘Palm Village’ eneo la Msasani Beach, Dar es Salaam.
Mradi huo unaohusisha ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kuuzia wananchi unatekelezwa na Kampuni ya GroupSix ya China ambayo pia inaadhimisha miaka 10 ya uwepo wake nchini.
Kwa hali hiyo, Samia ameitaka kampuni hiyo kuweka bei rafiki ili Watanzania wengi waweze kuzinunua nyumba hizo, jambo ambalo limesisitizwa pia na Ofisa Mwandamizi kutoka Ubalozi wa China nchini, Gou Haodong mapema wakati akizungumza katika hafla hiyo.
Ameipongeza kampuni hiyo kwa ubora wa kazi zake zilizofanyika katika kipindi cha miaka 10 walichokuwepo nchini wakifanya kwa pamoja na Watanzania na kuelezea matumaini yake kuwa kampuni hiyo itahamishia ujuzi na teknolojia kutoka kwa Wachina kwenda kwa Watanzania ili hatimaye waweze kuajiriwa na mashirika mengine au kujiajiri wenyewe.
“Naendeleza pongezi zangu...Kampuni ya Group Six, mmefanya kazi nzito kwa ubora wake, mradi ukikamilika mtalipa kodi kubwa hivyo kuongeza mapato,” alisema Samia na kuongeza; “Mradi utaongeza idadi ya mali zisizohamishika nchini, mali ambayo itaongeza thamani ya Tanzania na kutusogeza katika hatua ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii; kwa ujumla utachangia kukuza hadhi ya Taifa letu mbele ya uso wa dunia.”
Makamu wa Rais aliiambia kampuni hiyo kuwa serikali itatoa ushirikiano unaohitajika kuhakikisha mradi unakamilika kama ulivyopangwa kwa sababu urafiki kati ya Tanzania na China, ni urafiki wa kweli, haujawahi kuwa na vikwazo, masharti wala vigingi.
“Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) mpo hapa na Wizara ya Ardhi nawaagiza mhakikishe vikwazo vitakavyojitokeza katika utekelezaji wa mradi huu vinaondoka,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alisema mradi huo utagharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 70 mpaka utakapokamilika na kuiomba kampuni hiyo iangalie uwezekano wa kuwekeza katika ujenzi wa nyumba katika mikoa mingine nchini.
Mwijage aliieleza hadhara hiyo kuwa sekta ya ujenzi nchini imechangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa na kusema tafiti za takwimu za kiuchumi za kitaifa zinaonesha kuwa mwaka 2014 sekta ya ujenzi ilichangia asilimia 8.6 ya pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 6.4 kwa mwaka 2006 na kuifanya sekta hiyo kushika nafasi ya tatu kwa kuchangia pato la Taifa ikilinganishwa na sekta nyingine.
Pamoja na ujenzi wa “Palm Village” Kampuni ya Group Six imetekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba za biashara kama maduka makubwa, hoteli, nyumba za kuishi, shule ya Pwani Kusini, baadhi ya shule za sekondari za Zanzibar, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma.
chanzo;habarileo.
Comments