MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, amefuta likizo ya Mtendaji wa Mtaa wa Barabara ya Dodoma D, kata ya Mkimbizi, Manispaa ya Iringa, baada ya kukuta mtaa huo umetapakaa takataka ngumu.
Mkuu huyo wa mkoa alikumbana na hali hiyo wakati alipotembelea eneo hilo baada ya kupata malalamiko kutoka wananchi waliompigia simu juu ya uchafu kutozolewa.
Masenza alisema baada ya kutaarifiwa kuwa mtendaji huyo anakaimu nafasi ya mtendaji aliyeanza likizo, amemuagiza mkurugenzi wa manispaa kuifuta likizo hiyo mara moja na kurejea kuendelea na kazi kutokana na mtaa huo kukithiri kwa uchafu.
“Hali hii inatisha, inaonekana eneo hili hawafanyi usafi, sitavumilia hali hii na ndio maana nimeamua kufuta likizo yake arudi aje aniambie kwa nini aendelee kuwa mtumishi wa serikali kama eneo lake ambalo amepewa kusimamia hali iko hivi,” alisema Masenza.
Aidha, alimtaka Mtendaji wa Kata ya Mkimbizi, Tom Masinde, kumwelekeza mwenyekiti wa mtaa kuitisha mkutano wa wananchi na kuweka mipango ya kudumu ya usafi wa eneo hilo.
“Wananchi wenyewe wamesema hawajapendezwa na hali hii ya kuzagaa takataka na kulaumu viongozi wa mtaa kutochukua hatua licha ya kushauriwa mara kwa mara,” alisema.
chanzo;ippmedia.
Comments