MKUU wa Mkoa wa Mara, Magesa Mulongo, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga, kuhakikisha kwamba mashamba yote ya zao haramu la bangi yaliyopo katika wilaya hiyo yanabadilishwa kuwa alizeti ili kuinua uchumi na mapato ya wananchi wa mkoani humu.
Mulongo alitoa agizo hilo mjini hapa jana baada ya kumuapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Musoma, Humphrey Polepole.
Polepole aliteuliwa na Rais John Magufuli, hivi karibuni kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma kuziba pengo lililoachwa wazi na Zelothe Stephen, aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Machi 12, mwaka huu.
Mulongo alisema kutokana na baadhi ya wananchi wilayani Tarime kutafuta fedha kwa njia haramu, wamejingiza katika kilimo cha bangi kwa njia ya kificho huku kilimo hicho kikiaminiwa kufadhiliwa na baadhi ya wafanyabiashara kutoka nchi jirani ambako inadaiwa kuwa na soko kubwa.
Alisema anataka kuiona Wilaya ya Tarime ikiwa ni ghala kuu la chakula kwa wananchi wa Mkoa wa Mara, hivyo kilimo haramu cha bangi kilichoshamiri na kuota mizizi kwa zaidi ya miongo miwili, sasa kinatokomezwa na wananchi kuwa na mtazamo chanya wa kujihusisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Aidha, amewatahadharisha wananchi wa Mkoa wa Mara kutambua kuwa serikali haina mpango wa kuwaletea chakula cha msaada kukabiliana na upungufu utakaojitokez.
Kwa msingi huo aliwahimiza kuweka bidii katika kilimo cha zao la muhogo linalostahimili ukame na kuagiza kila kaya kuanza maandalizi ya kulima ekari mbili kuanzia Jumatatu ijayo.
Alionya kwamba watakaozembea agizo hilo watalima kwa nguvu ya dola.
Kadhalika, Mulongo amewaagiza wenyeviti na watendaji wa vijiji katika wilaya hiyo kuanza mara moja operesheni maalum ya kusaka mashamba ya bangi.
Amewaonya kwamba wale wote ambao maeneo yao yatabainika kuwa na mashamba hayo, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwavua kwanza nyadhifa zao kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Luoga alisema agizo la Mkuu wa Mkoa limekuja wakati mwafaka.
Alisema serikali wilayani Tarime kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama, imeshang’oa zaidi ya ekari 20 za bangi wilayani humo ikiwa ni hatua ya kupambana na kilimo cha zao haramu.
chanzo;ippmedia.
Comments