SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema italazimika kuzibomoa zaidi ya nyumba 300 zilizojengwa katika njia inayopitisha maji na maeneo ya mabondeni na hivyo kusababisha mafuriko mara kwa mara.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua wananchi waliokumbwa na mafuriko kutokana na mvua za masika zinazoendelea nchini.
Aboud alisema njia pekee ya kuondokana na tatizo la mafuriko katika kipindi cha mvua za masika ni kubomoa nyumba zilizojengwa katika vyanzo vya maji au njia zinazopitisha maji ya mvua na kuwa chanzo cha mafuriko.
“Tutalazimika kuvunja nyumba zipatazo 300 ambazo zimejengwa katika maeneo mbalimbali ambayo yamekuwa yakipitisha maji au vyanzo vya maji katika maeneo ya mabonde kama ndio njia pekee ya kukabiliana na mafuriko ya mara kwa mara,” alisema.
Alisema kutokana na mvua za masika zinazoendelea ambazo zimetabiriwa kuwa kubwa na taasisi za hali ya hewa zaidi ya watu 900 wameathirika ma mvua hizo na kulazimika kuzihama nyumba zao na kuishi kwa majirani.
Maeneo ambayo yameathirika zaidi ni Mwanakwerekwe karibu na soko kuu, Jang’ombe pamoja na Sebleni ambapo zaidi ya wakazi 30 walilazimika kuzihama nyumba zao, baada ya kuingiliwa na maji ndani ya nyumba zao.
“Hili bwawa lililopo Sebleni linatakiwa kufanyiwa kazi na serikali ikiwemo kuweka mitaro zaidi ingawa tatizo lipo kwa wananchi kuchota mchanga kwa kasi kubwa kwa matumizi ya ujenzi wa nyumba,” alisema Talib Ussi ambaye ni mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima aliyelazimika kuhama katika makazi yake.
chanzo;habarileo.
Comments