Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amekabidhi gari la kubebea wagonjwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma, lenye thamani ya Sh. milioni 77.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi gari hilo kwa Katibu Tawala wa mkoa huo, Hassan Bendeyeko, Waziri Mhagama aliwataka walitunze na kulitumia kwa ajili ya malengo yaliyokusudiwa tu.
“Gari hili ni jipya kabisa, likitunzwa litadumu kwa hiyo tunawaomba mlitunze na kuhakikisha linatumiwa kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo,” alisema Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho (CCM).
Mhagama alikabidhi gari hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mhagama alisema anamshukuru Waziri Mkuu ambaye ametoa gari hilo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa Januari 5, mwaka huu wakati akizungumza na madaktari, wauguzi na watumishi wengine wa hospitali ya rufaa ya mkoa huo.
Waziri Mkuu alifanya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Ruvuma ambapo alitembelea na kukagua Hospitali ya Rufaa ya mkoa na baadaye kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo.
Akitoa shukrani mara baada ya kukabidhiwa gari hilo, Katibu Tawala wa mkoa Bendeyeko alisema kipekee wanashukuru kupatiwa gari la wagonjwa kwani ilikuwa vigumu kwao kuitatua changamoto hiyo.
“Ziko changamoto nyingi zinazoikabili hospitali yetu ambazo tuliziwasilisha kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini hii ya gari ilikuwa nje ya uwezo wetu kwani kama mkoa tusingeweza kuimudu kutokana na ufinyu wa bajeti," alisema.
"Tunashukuru sana na tunaahidi kulitunza gari hili.”
Alisema kupatikana kwa gari hilo kutasaidia kuboresha huduma za tiba hasa ikizingatiwa kuwa mkoa huo hauna hospitali ya manispaa, kwa hiyo hospitali ya rufaa inalazimika kuhudumia wagonjwa kutoka kwenye manispaa pamoja na wilaya ya Namtumbo.
chanzo;ippmedia.
Comments