Mfumo wa Opras kuanza Julai.

SERIKALI inatarajia kuanza utekelezaji wa mikataba ya utendaji kazi katika mwaka wa fedha 2016/17.
Sambamba na hilo, mfumo wa wazi wa upimaji wa utendaji kazi (Opras) utawezesha serikali kupima utendaji kazi kwa kila taasisi ya umma kila mwaka.
Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angellah Kairuki, wakati akijibu swali la Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua mwaka 2002 serikali ilipitisha Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na marekebisho yake ya mwaka 2008 yaliyoweka mfumo wa wazi wa upimaji na ujazaji wa mkataba wa utendaji kazi (Opras), hivyo ni kwa kiasi gani mfumo huo umetekelezwa na lini mfumo wa kupima taasisi utaanzishwa na kutangazwa hadharani.
Kairuki alisema mfumo huo ulianzishwa Julai, 2004 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kutekeleza sera ya menejimenti na ajira katika utumishi wa umma ya mwaka 1998 kama ilivyohuishwa mwaka 2008 pamoja na sheria ya utumishi wa umma sura 298.
Alisema katika mwaka wa fedha 2011/12 na mwaka 2013/14 Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma, ilifanya tathmini ya uzingatiaji na utekelezaji wa mfumo huo katika taasisi za umma.
“Thathmini hiyo ilihusisha taasisi za umma 139 katika awamu mbili. Awamu ya kwanza ilihusisha taasisi za umma 110 na awamu ya pili ilihusisha taasisi 29 ambayo ililenga kufuatilia taasisi zilizokuwa na utekelezaji wa kiwango cha juu katika awamu ya kwanza, matokeo ya tathmini hii yalionyeshwa utekelezaji uko asilimia 51,” alisema.
Alibainisha hatua zilizochukuliwa ili kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa na watumishi wote, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora imewaagiza waajiri kuhakikisha mtumishi atapandishwa cheo kwa kuzingatia matokeo ya Opras.
Alisema hatua hiyo imesaidia kuongeza kiwango cha utekelezaji kwa kuwa kila mtumishi sasa anatekeleza mfumo huo kama sharti la kupandishwa cheo.
Kuhusu lini serikali itaanza kutangaza mfumo wa kupima taasisi, Kairuki alisema utaanza katika mwaka wa fedha 2016/17 na mikataba hiyo itatekelezwa na taasisi zote za umma ikiwa ni pamoja na wizara, idara zinazojitegemea na wakala za serikali.
Zingine, kwa mujibu wa Kairuki, ni sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa, mashirika na taasisi za umma.
chanzo;ippmedia.

Comments