WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, kimepungua kwa asilimia 2.5 na kwamba Serikali itaendeleza juhudi za kuvutia uwekezaji ili kupunguza zaidi kiwango hicho.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana mchana wakati akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.
“Utafiti wa hali ya ajira nchini wa mwaka 2014 umeonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3 mwaka 2014. Aidha, ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014,” alisema.
Waziri Mkuu amesema moja ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira ni vijana kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi nchini.
“Programu hiyo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi kutoka asilimia tatu ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha uchumi wa viwanda. Vilevile, kupunguza idadi ya watu wenye kiwango cha ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 54,” alisema.
Aliwaagiza watendaji wakuu wa wizara, idara zinazojitegemea, wakala za Serikali, taasisi za umma, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha kuwa ukuzaji wa ajira unakuwa ajenda ya msingi ya kudumu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
chanzo;habarileo.
Comments