Hospitali zaagizwa kutofuja mapato.

HOSPITALI zinazotumia mfumo wa ukusanyaji mapato wa kielektroniki zimetakiwa kutobweteka na mapato yanayokusanywa kila siku, na badala yake ziwe makini katika matumizi.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ambayo kupitia mfumo huo mpya, inakusanya Sh milioni 500 kwa mwezi.
Alisema ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa kielektroniki unasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuboresha huduma za afya nchini, ikiwemo ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba na utoaji wa motisha kwa watumishi.
“Bado tunatambua hali ya uhaba wa dawa na vifaa tiba kuanzia ngazi zote, tukiweza kusimamia vizuri hili tutafanikiwa,” alisema.
Aidha, alisema wanatarajia bajeti ya dawa itaongezeka zaidi ya mara tatu kulinganisha na bajeti za nyuma, hivyo wameishauri MSD inunue dawa kutoka kwa wawekezaji wa nchini akisema itakuwa na bei nafuu na itaongeza tija na upatikanaji wa dawa kwa haraka.
Aidha, ameutaka mkoa kufuatilia, kuwafichua na kuwachukulia hatua watu watakaojihusisha na wizi wa dawa.
“Tunao watumishi wachache wa afya ambao wanahujumu na kuiba dawa na kuzipeleka kwenye maduka binafsi ya dawa, hao hatutowafumbia macho na kuwapeleka mahakamani,” alisema.
Akizungumzia upungufu wa watumishi wa kada ya afya nchini, alisema nchi ina upungufu wa asilimia 52, hivyo serikali inatarajia kuajiri watumishi takribani 10,000 hivi karibuni ambao watatawanywa nchi nzima ikiwemo mikoa iliyo pembezoni. Hospitali ya kanda ya rufaa Mbeya inakusanya kwa mwezi kiasi cha Sh milioni 500, inahudumia mikoa saba nchini na kuhudumia zaidi ya watu milioni mbili.
chanzo;habarileo.

Comments