Ghasia za chuki dhidi ya wageni zaendelea Zambia, Wanyarwanda wachomwa moto.

Mji mkuu wa Zambia Lusaka umeendelea kushuhudia ghasia za chuki dhidi ya wageni na ripoti zinasema raia wawili wa Rwanda wameuawa kwa kuchomwa moto.
Ghasia hizo za kulalamikia uwepo wa wageni katika mji mkuu wa Zambia Lusaka zilizoibuka siku ya Jumatatu zinaendelea kushuhudiwa katika maeneo mengi ya mji huo na kuzusha wasiwasi mkubwa kwa raia wa kigeni walioko katika mji huo.
Siku ya Jumanne zaidi ya watu 200 walitiwa mbaroni katika mji wa Lusaka huku maandamano ya ghasia na wizi ukiendelea kushuhudiwa.
Makumi ya maduka yanayomilikiwa na raia wa Rwanda yameporwa kufuatia madai kwamba raia wa Rwanda wamekuwa wakishiriki katika mauaji ya kishirikina.
Takriban watu saba wameuawa katika wiki za hivi karibuni na viungo vyao vya mwili kukatwa.
Inadaiwa kwamba, viungo hivyo hutumika kufanyia uchawi.
Kuna zaidi ya wakimbizi 7000 wa Rwanda nchini Zambia.
Wengi wao wamedaiwa kutoroka maduka na makaazi yao.
Baadhi ya raia wa kigeni wamelazimika kukimbilia katika vituo vya polisi kuokoa maisha yao.
Serikali ya Zambia imetangaza kuwa, vyombo vya usalama vinadhibiti hali ya mambo na kuwahakikishia raia wa kigeni kwamba, usalama wao utalindwa.
chanzo;kiswahili.irib.ir.

Comments