MAOFISA wawili wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini (TFS) na wafanyabiashara watano, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyerembe Mnasa, kwa tuhuma za kukutwa na shehena ya magogo, mbao na mkaa inayodaiwa kusafirishwa nje ya nchi kinyume cha sheria.
Watuhumiwa hao walikamatwa jijini Mbeya jana baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kuambatana na maofisa wa TFS kutoka makao makuu na kufanya msako wa kushtukiza kwenye maghala ya wafanyabiashara hao jijini Mbeya na kufanikiwa kukamata shehena ya mazao ya misitu ikiwa imefichwa.
Aidha, katika ukaguzi huo, walimfumania mmoja wa wafanyabiashara hao akipakia mkaa kwenye gari aina ya Fuso, ikiwa ni maandalizi ya kuusafirisha mkaa huo hadi jijini Dar es Salaam ambako inadaiwa inagepakiwa kwenye meli na kupelekwa nchini China.
Katika ukaguzi huo pia walikamata magogo na mbao zenye ukubwa tofauti, bidhaa ambazo wamiliki wake walipotakiwa kutoa nyaraka zinazoonyesha uhalali wake hawakuwa nazo.
Hata hivyo, magogo yote yaliyokamatwa yalikuwa yamegongwa mhuri wa serikali ukionyesha kuwa magogo na mbao hizo zilivunwa wilayani Chunya na kwa baraka za Wakala wa Huduma za Misitu nchini.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Munasa alisema kitendo cha kupatikana kwa magogo hayo kwenye maghala ya wafanyabiashara huku maofisa wa TFS waliopo jijini Mbeya wakiwa hawana habari, kinaonyesha jinsi watendaji wa serikali walivyo wazembe.
“Haiwezekani mali yote hii ihifadhiwe hapa bila maofisa wa TFS ambao ndiyo tumewapa dhamana ya kulinda rasilimali zetu hawajui, naagiza wote tuliowakamata pamoja na mofisa wetu wa TFS, wakamatwe wakatoe maelezo Polisi kuhusu rasilimali hizi,” alisema Munasa.
Aliliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata mara moja maofisa hao pamoja na wafanyabiashara waliokutwa na mazao hayo ya misitu ili wakatoe maelezo, sambamba na kuhakiki bidhaa hizo kama ni halali.
Alisema serikali ya awamu ya tano hairuhusu aina yoyote ya hujuma za rasilimali za Taifa, kwani ni mali ya Watanzania wote, hivyo zinapaswa zitumike kwa manufaa ya wananchi wote.
Aidha, aliwaagiza wataalam kupitia nyaraka zote zitakazoletwa na wafanyabiashara hao na pia kuchunguza mhuri uliogongwa kwenye mbao hizo ili kubaini kama uvunaji wa mazao hayo ulizingatia sheria za nchi.
Maofisa wa TFS kutoka Makao Makuu jijini Dar es Salaam, walisema kuwa walipata taarifa za uwapo wa mazao hayo ya misitu kutoka kwa raia wema na kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kila wanapoona rasilimali za taifa zikihujumiwa.
Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Misitu, Deusdedit Bhwoyo, alisema kuwa taarifa za uwapo wa rasilimali hizo waliletewa wananchi wakiwa Dar es Salaam na ndipo walipoamua kusafiri kimya kimya hadi Mbeya kushughulikia suala hilo.
Alisema walipofika Mbeya, walimshirikisha Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, ambaye aliwapatia ushirikiano mkubwa uliofanikisha kukamatwa kwa rasilimali hizo kwa kiwango kikubwa kinyume cha matarajio yao.
Kaimu Meneja wa TFS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Deusdedit Mloge, alisema kwa kuwa magogo hayo yana mhuri wa serikali, inawezekana yalivunwa kihalali, ingawa mhuri pekee hautoshi kuhalalisha umiliki wa mbao hizo.
Mloge ambaye pia ni miongoni mwa maofisa waliokamatwa kwa ajili ya mahojiano na Polisi, alisema mbele ya Mkuu wa Wilaya kuwa kazi ya mamlaka hiyo ni kupiga mihuri kwenye mbao na magogo pamoja na kutoa kibali cha kusafirisha mazao ya misitu kwa watu wanaojihusisha ba biashara hiyo, lakini hawatoi leseni ya uvunaji.
Alisema kuwa suala la utoaji wa leseni za uvunaji wa mazao ya misitu linashughulikiwa katika ngazi ya halmashauri ya wilaya, hivyo huenda chanzo cha tatizo hilo kikawa kwenye halmashauri ambako mbao na mkaa huo vilivunwa.
chanzo;darwaya.
Comments