WILAYA YA CHAKE CHAKE.
WAJUMBE wa kamati tendaji ya hifadhi ya mkondo wa Pemba ‘PECA’ wametakiwa kurudi katika maeneo yao kiwilaya kupendekeza wajumbe watakaoshirikishwa katika uundwaji wa kamati za uhifadhi wa samaki walio katika mpango.
Hayo yameelezwa na Ofisa Mdhamin, Wizara ya mifugo na uvuvi, Bi Mayasa Hamad Ali, wakati wa akifungua kikao cha kamati tendaji na wajumbe wa mradi wa ‘Swiofish’ uliofanyika Wesha , Chake Chake P emba.
Amesema malengo makuu ya kufanya vikao hivyo ni pamoja na kushauriana na kuelekezena taratibu za utekelezaji wa kazi kwa nia ya kuuenzi mradi ,ili uweze kudumu kwa faida ya jamii nzima.
Ofisa Mdhamin ameeleza kuwa kila wilaya watachaguliwa watu tisa katika makundi matatu yaliopewa kipaumbele cha hifadhi wakiwemo wataalamu wa uvuvi wa pweza, samaki wa kuelea na wanaoishi kwenye matumbawe.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya uvuvi Pemba, Sharif Mohammed Faki, amesema kazi inayofuata kwa sasa ni uteuzi wa wajumbe wa kamati kiwilaya, ili kujadili kamati zitakazosimamia uhifadhi.
Sharif, ameeleza kuwa, wajumbe watakao teuliwa ni kulingana na aina ya samaki waliopewa kipaombele baada ya kupendekezwa vijiji vinavyojulikana kwa shughuli za uvuvi kwa kuwashirikisha wavuvi wenyewe kupitia mikutano .
Akitoa mapendekezo yake, mwenyekiti wa kamati za uvuvi wilaya ya Wete, Mohammed Kombo Hamad, amesema ni vyema kwa watendaji kupendekeza wajumbe kulingana na aina ya ujuzi wa uvuvi walionao.
Katibu wa PECA Pemba Khamis Sharif Haji, amesema kuwa kamati zitakazo chaguliwa lazima ziwashirikishe watumishi wa wilaya, ili ziweze kutambulika vyema na jamii.
Nae mwenyekiti wa wavuvi wilaya ya Micheweni, Mkubwa Said Ali amesema kufanya mikutano na wavuvi ni jambo jema litakalosaidia ushirikishwaji wa kuwateua wajumbe wanaofaa , ili kuepusha mivutano na jamii.
Mradi wa ‘Swiofish’ni mradi wa kikanda ikiwemo Komoro, Mozambiq, Tanzania, na utakua na ushirikiano wa kuhifadhi na kusimamia viumbe wa bahari na utafanyakazi kwa vijiji 60 ndani ya Zanzibar.
MWISHO.
Comments