VYOMBO vya habari vimetakiwa kuelimisha wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa kipindupindu ambao tangu uanze miezi saba iliyopita bado upo na unazidi kuenea na kusababisha vifo.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mratibu wa Ufuatiliaji na Udhibiti wa magonjwa ya mlipuko mkoani Dodoma, Gerald Manasseh wakati wa semina ya waandishi wa habari.
Alisema vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii juu ya chanzo cha ugonjwa, dalili, ueneaji wake, athari zake, jinsi ya kujikinga na namna ya kumhudumia mgonjwa.
Akitoa mfano alisema katika redio kuna vipindi vya afya ambavyo vinaweza kutumika kuelimisha jamii ili kuweza kutokomeza ugonjwa huo ambao bado unaendelea kuwepo tangu ulipozuka Agosti mwaka jana.
“Kipindupindu kipo Dodoma huu ni mwezi wa saba tangu kianze wananchi wanaougua, wanapoteza maisha lazima tufanye kitu hapa ili jamii ipate elimu ipone,” alisema.
Pia alisema katika wilaya za mkoa wa Dodoma wananchi walioathirika na ugonjwa huo asilimia kubwa ni wale wanaotumia maji kutoka vyanzo ambavyo si rasmi.
“Wengi hawana mazoea ya kuchemsha maji kabla ya kunywa jambo ambalo ni hatari sana,” alisema.
Alisema kati ya Machi 12 – 22 kulikuwa na wagonjwa wapya 92 wa kipindupindu huku waliofariki wakiwa watatu. Hata hivyo, alisema sasa wamebaki wagonjwa saba.
Semina hiyo iliyoendeshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kushirikiana na hospitali ya mkoa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imevitaka vyombo vya habari kufanya kazi zake bila kujali vinalipwa nini ili kuutokomeza ugonjwa huo katika mkoa wa Dodoma.
Kwa upande wake, Ofisa Afya na Mazingira kutoka TAMISEMI, Stella Kajange alisema ugonjwa wa kipindupindu uko mkoani Dodoma tangu Agosti mwaka jana na sababu kubwa zinazofanya uendelee kuenea ni uelewa mdogo wa wananchi.
chanzo;habarileo.
Comments