Vyama vilivyoshiriki uchaguzi Zanzibar kuteta na mabalozi.

Umoja wa vyama vya siasa visivyokuwa na uwakilishi Bungeni, unatarajia kuandaa meza ya mazungumzo yatakayowashirikisha mabalozi, taasisi za kimataifa na nchi wahisani kwa lengo la kushauriana na kuwapa sababu ni kwa nini vyama hivyo viliamua kushiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar.
Vyama vinavyounda umoja huo ni CCK, DP, SAU, AFP, TLP, UPDP, NRA, UMD na Demokrasia Makini.
Akizungumza na chanzo hichi cha habari jana, Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi,alisema watafanya mazungumzo hayo kwa sababu wanaamini kuwa  matatizo ya kisiasa nchini yatatatuliwa na Watanzania wenyewe na si vinginevyo.
Muabhi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Makatibu Wakuu wa Vyama Visivyo na Wabunge, alisema watafanya mazungumzo na mabalozi na taasisi za kimataifa kwa sababu ni muhimu kujenga uhusiano na kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na taasisi hizo.
“Hatuwezi kusema kwamba uchaguzi Zanzibar umekwisha tukaishia hapo. Zanzibar bado kuna tatizo kubwa la kisiasa ambalo ni lazima litafutiwe ufumbuzi,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi visiwani Zanzibar, matarajio yao ni kuona jitihada za Rais Dk. Ali Mohammed Shein, akishirikisha wadau wote wa kisiasa walioshiriki uchaguzi huo katika kutafuta muafaka wa kudumu wa kuondokana na migogoro ya kisiasa inayojitokeza visiwani humo.
Mabalozi wamekuwa na msuguano na Serikali ya Zanzibar kwa kupinga kitendo cha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana kwa kile wanachodai kuwa ulikuwa huru na haki.
Januari 29, mwaka huu Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya (EU) inayojumuisha nchi za Ubelgiji, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi na Uingereza zenye ubalozi nchini, zilitoa tamko la pamoja la kumtaka Rais Dk. John Magufuli, kuingilia katika mgogoro huo.
“Tunamtaka Rais Magufuli kuonyesha uongozi wake kupitia mgogoro huu wa kisiasa kwa kuingilia kati na kutafuta usuluhishi baina ya vyama vikuu kuhakikisha amani pande zote,” ilisema sehemu ya tamko hilo.
Tamko hilo pia lilieleza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa na kasoro zilizoelezwa na kwamba waangalizi wa kutoka Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki, EU, Marekani na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) waliridhika na mwenendo wa uchaguzi huo.
Tamko hilo lilisisitiza kurejewa kwa mazunguzo ya vyama vinavyovutana na kuwa na maridhiano kuliko kurudi kwenye uchaguzi mpya.
Walisema kurudiwa kwa uchaguzi huo kutaongeza hali ya wasiwasi visiwani humo, hivyo ni vyema pande zote (CUF na CCM) zikakutana na kuwa na makubaliano ya pamoja na ya amani.
chanzo;ippmedia.

Comments