Serikali yabebeshwa lawama.



Baada ya Marekani kupitia Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), baadhi ya vyama vya siasa nchini vimesikitishwa na hali hiyo na kuitaka serikali kutatua changamoto zilizosababisha kutokea kwa hali hiyo.
 
Juzi Bodi ya Wakurugenzi ya MCC ilifanya kikao nchini Marekani na kuijadili Tanzaia, baada ya kushindwa kukidhi mashariti iliyoyatoa, ikiwamo kutatua mgogoro wa Zanzibar na sheria ya makosa ya mtandao.
 
Wakizungumza na Nipashe, viongozi hao wa vyama vya siasa nchini, walisema jana kuwa kitendo hicho kimeidhalilisha nchi kwa sababu vyama vya upinzani vilikuwa vinakemea matendo hayo yaliyosababisha nchi kuvuliwa uanachama tangu awali.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanznaia Bara), Magdalena Sakaya, alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za Tanzania kuondolewa katika nchi zinazonufaika na shirika hilo.
 
Alisema hatua hiyo ni udhaifu mkubwa kwa taifa kwa sababu tangu awali, vyama vya upinzani vimekuwa vikipiga kelele kuhusu uonevu unaofanywa katika uchaguzi wa Zanzibar na sheria ya makosa ya mtandao.
 
“Tangu bungeni wabunge tumekuwa tukipiga kelele, lakini wakawa wanatupuuza, sasa matokeo yake yametokea. Nchi imekosa fedha na wananchi wanakwenda kutaabika,”alisema Sakaya.
 
Alisema Tanzania bado inahitaji wahisani katika kuendesha miradi yake ya maendeleo hivyo kuondolewa MCC kutaleta athari nyingi.
 
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alisema uamuzi uliotolewa na MCC ulitarajiwa muda mrefu kwa sababu serikali ya Tanzania haikutaka kushughulikia mapema.
 
Alisema kilichotokea Zanzibar ni uongo mkubwa, kwa sababu CCM imenyang’anya ushindi ambao ulitakiwa kwenda kwa CUF. Aliongeza kuwa kuondolewa MCC kunaifundisha Tanzania kufuata misingi ya demokrasia na utawala bora.
 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabhi, alisema kwa sasa Tanzania imeshapoteza uhusiano wa kimataifa na taasisi za kimataifa.
 
Alisema Tanzania kuondolewa MCC kutakuwa kumetoa funzo kuwa haipasi kuishi kwa kupiga magoti na kuomba.
 
Alisema kwa sasa Tanzania inapaswa kujitegemea na kujenga miundombinu ya kiuchumi na serikali ya Tanzania inatakiwa kusimama imara na kutoruhusu mataifa ya Ulaya na washirika wao kuiendesha nchi ambayo ina serikali yake na watu makini.
 chanzo;ippmedia.

Comments