Profesa Mbarawa alitaka Shirika la Posta kujipanga

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amelitaka Shirika la Posta kujipanga na kujiimarisha kutokana na utandawazi uliopo kuendana na hali halisi ya maisha ya sasa ili kukabiliana na ushindani uliopo.
 
“Lazima ndugu zangu watu wa Posta mjipange na kujiimarisha kwa kuwa hivi sasa kuna ushindani mkubwa sana kutokana na utandawazi, lakini pia muwe wabunifu kwa kuhakikisha mnatoa huduma zenu kwa wakati ili kuongeza idadi ya wateja,” alisema Waziri Profesa Mbarawa akiwa katika ziara ya siku tatu mkoani Tanga mwishoni mwa wiki.
 
Awali, Meneja wa Shirika la Posta Tanzania mkoani Tanga, Rehema Marijani, wakati akisoma taarifa yake kwa Waziri 
Profesa Mbarawa, alisema usafirishaji wa mifuko ya barua ni changamoto kubwa kwa Wilaya za Kilindi na Pangani mkoani Tanga.
 
Marijani alisema changamoto hiyo inazidi kuwa kubwa hasa kipindi cha mvua kutokana na miundombinu ya barabara isiyokuwa mizuri na hivyo kusababisha ucheleweshwaji mkubwa kuwafikia wateja wao.
 
Marijani alisema hali hiyo inatokana na wenye vyombo vya usafiri pia kutokukubali kubeba mifuko ya Posta inayokwenda maeneo hayo nyakati za mvua na wale wanaokubali wanataka fedha nyingi ambazo haziendani au hazilingani na thamani ya mzigo halisi unaosafirishwa kwa wakati huo.
 
“Mheshimiwa Waziri, hali hii imekuwa ni changamoto kubwa sana kwetu kufikisha barua hizo kwa wakati hasa nyakati za mvua, lakini tunaangalia namna ya kukabiliana nayo,” alisema.
 
Aidha, alisema baadhi ya ofisi za wilaya ambazo zimeanza hivi karibuni hazina majengo na hivyo kulazimika kukodi majengo kuongeza gharama.
 
"Tunalazimika kukodi majengo ya watu binafsi ambapo inaongeza gharama za uendeshaji," alisema.
chanzo;ippmedia.

Comments