Jumatano, Machi 16, 2016
Leo ni Jumatano Leo 6 Jamadi Thani 1437 Hijria sawa na 16 Machi 2016.
Katika siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, sawa na tarehe 26 mwezi Esfand mwaka 1373 Hijria Shamsiya aliaga dunia Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ahmad Khomeini, mwana wa Imam Ruhullah Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Sayyid Ahmad Khomeini alizaliwa mwaka 1324 Hijria Shamsiya katika mji mtukufu wa Qum nchini Iran na kuanza kujifunza elimu ya kidini kwa baba yake. Sayyid Ahmad Khomeini alikuwa na nafasi muhimu katika kuwaunganisha wanamapinduzi na Imam Khomeini wakati wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita, alifariki dunia Bi Selma Lagerlof mwandishi wa Sweden. Lagerlof alizaliwa mwaka 1858 na baada ya kumaliza masomo yake akaanza kujishughulisha na ukufunzi na uandishi wa hadithi na hekaya. Lagerlof alikuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Nobel katika fani ya fasihi mwaka 1909.
Na siku kama ya leo miaka 157 iliyopita Alexander Stepanovich Popov, mvumbuzi na mwanafizikia wa Russia alizaliwa. Baada ya kuhitimu masomo yake katika taaluma ya fizikia, alianza kujishughulisha na ufundishaji katika vyuo vikuu vya nchi hiyo. Mbali na shughuli hiyo, Popov aliendelea mbele na utafiti wake katika nyanja mbalimbali za kielimu ambapo baadaye alifanikiwa kuvumbua chombo cha kunasia sauti na kukipa jina la kinasia sauti. Aliaga dunia mwaka 1906.
Comments