Jumatano 23 Machi, 2016
Leo ni Jumatano tarehe 13 Jumadi Thani 1437 Hijria sawa
na Machi 23, 2016.
Tarehe 13 Jumadithani mwaka 64 Hijria alifariki dunia
Fatima
bint Hizam al Amiriyya al Kilabiyya, maarufu kwa laqabu ya
Ummul Banin, mke mwema na mcha Mungu wa Imam Ali bin Abi Twalib (as).
Wanahistoria wamehitilafiana juu ya siku aliyozaliwa na baadhi wanasema alizaliwa mwaka wa 5 baada ya Hijra ya Mtume (saw).
Imam Ali bin Abi Twalib alimuoa bibi huyu mwema baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as).
Ummul Banin anatoka katika kizazi cha mashujaa wakubwa wanaopigiwa mfano baina ya Waarabu. Baada ya kuolewa, mtukufu huyo alimuomba Imam Ali ampe laqabu ambayo atakuwa akiitumia kumwitia badala ya jina lake la Fatima ambalo alichelea kwamba litakuwa likiwakumbusha wajukuu wa Mtume mama yao, yaani Fatimatu Zahraa (as).
Aliwapenda sana Ahlul Bait wa Mtume na historia inahadithia jinsi alivyowatuma wanae wote wanne kwenda kulinda familia ya Mtume hususan Imam Hussain katika ardhi ya Karbala. Watoto wote wanne wa Hadhrat Ummul Banin, wakitanguliwa na Abul Fadhl al Abbas, waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kaka yao Hussein katika medani ya Karbala. Ummul Banin alifariki dunia katika siku kama ya leo mjini Madina na kuzikwa katika makaburi ya Babii.
Siku kama ya leo miaka 1007 iliyopita alifariki dunia Ibn Haytham, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu katika mji wa Cairo.
Ibn Haytham alizaliwa mwaka 354 Hijiria katika mji wa Basra kusini mwa Iraq. Alibobea katika elimu za fizikia, tiba, falsafa na unajimu.
Mwanazuoni huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya hisabati, nujumu na tiba.
Moja ya vitabu vyake muhimu ni al-Manadhir ambacho kimetafsiriwa katika lugha ya Kiingereza na kinatumika katika elimu ya nujumi.
Siku kama hii ya leo miaka 66 iliyopita lilianzishwa Shirika la
Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Shirika hilo liko chini ya Umoja wa Mataifa na lina ushirikiano wa kudumu na taasisi zote za hali ya hewa duniani.
Moja kati ya malengo ya Shirika la Hewa Duniani ni kustafidi kadiri inavyowezekana na sayansi ya hali ya hewa katika masuala ya anga, ubaharia, kilimo na katika shughuli nyinginezo za kibinadamu na pia kusaidia juhudi za kuboresha takwimu na taarifa za hali ya hewa duniani.
Na miaka 60 iliyopita katika siku kama hii ya leo katiba mpya ya Pakistan ilibuniwa na kwa mujibu wake utawala wa nchi hiyo ulibadlishwa kutoka utawala wa gavana mkuu na kuwa na mfumo wa Jamhuri.
Nawabzada Liaquat Ali Khan Waziri Mkuu wa wakati huo wa pakistan alichukua madaraka ya kuiongoza nchi hiyo mwaka 1948 kufuatia kifo cha Muhammad Ali Jinnah aliyekuwa mwasisi na gavana mkuu wa nchi hiyo.
Liaquat Ali Khan naye pia aliuawa na raia mmoja wa Afghanistan mwaka 1951.
Comments