KUKOSEKANA kwa kiwango cha madini ya vikositi na krujina katika mwani ni miongoni mwa changamoto inayopelekea kushuka kwa bei ya kilimo hicho kwa kukosa tija, jambo ambalo limekuwa ni kikwazo kwa wakulima.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika kijiji cha Mjinikiuyu shehia ya Kiuyu Minungwini, Afisa manunuzi wa kijiji hicho katika Kampuni ya ‘C-WEED CORPORATION’ Omar Faki Hassan alisema, bei ya mwani hushuka kutokana na kukosa kiwango kinachotakiwa na makampuni makubwa yanayonunua.
Alisema kuwa, wapo baadhi ya wakulima wa kilimo hicho wamekuwa wakifanya udanganyifu wakati wanapouza mwani, kwa kuutia maji ndani yake ili uwe mzito, jambo ambalo linakosa kiwango kinachotakiwa.
Alieleza kuwa, mwani hutumika kutengenezea vitu mbali mbali ikiwemo juisi, hivyo unapokosa kiwango, madini yanayotakiwa hayawezi kupatikana na kupelekea kushuka kwa bei hiyo.
Afisa huyo, aliwataka wakulima hao kuzidisha bidii ya kulima mwani na kuuza ukiwa na viwango vinavyotakiwa, ili kuweza kuipandisha bei ya ukulima huo.
Mapema wakulima wa mwani katika kijiji hicho, walisema kuwa wamekuwa wakilima mwani kwa muda mrefu sasa, bila ya kupata kipato cha kujikimu kimaisha, jambo ambalo linawarudisha nyuma kimaendeleo.
Mmoja wa wakulima hao, Time Abdalla Ali (50) mzaliwa wa kijiji hicho alieleza kuwa, wamekuwa wakichukua jitihada za kulima mpaka kuvuna ukiwa safi, ingawa bei bado imekuwa ndogo sana ukilinganisha na kazi yenyewe.
Kwa upande wake Mgeni Makame Othman (35) alisema hana kazi nyengine zaidi ya ukulima wa mwani, hivyo huitunza ili waweze kupata fedha zitakazowakwamua na umasikini ingawa wanakwama.
Nae Saada Massoud Hamad alisema kuwa, mwani ndio tegemeo lao kubwa katika kijiji hicho na kuziomba kampuni zinazonunua kuwaangalia kwa jicho la huruma na kuweza kuwasaidia.
Wananchi wa kijiji cha Mjinikiuyu shehia ya Kiuyu Minungwini Wilaya ya Wete Pemba, wanakabiliwa na uhaba wa bei ya kununulia mwani, ambapo Afisa manunuzi wa kijiji hicho alisema sababu kubwa ni kukosekana kwa kiwango kinachotakiwa na makmpuni.
Comments