Halmashauri zatakiwa kuilipa TSN
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura ameziagiza halmashauri zote nchini, kutenga bajeti maalumu na kulipa madeni ya matangazo, wanayotolewa magazetini kupitia Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN) ili kuwezesha kampuni hiyo kuweka kupata maendeleo zaidi.
Aidha, Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Kanda ya Kaskazini, Christopher Mkama amesema shirika hilo hadi mwezi ujao, litakuwa limerekebisha masafa ya urushwaji wa matangazo katika mikoa na wilaya zinazopakana na maeneo mbalimbali ya mipaka ya nchi ili matangazo ya redio yasikike vizuri, badala ya hivi sasa baadhi ya wananchi wa mipakani kupata matangazo ya redio za nchi nyingine zilizo karibu na mipaka ya nchi.
Wambura alitoa rai hiyo jana wakati alipotembelea ofisi za magazeti ya TSN ya Daily News na HabariLeo jijini Arusha; na ofisi za TBC Kanda ya Kaskazini na maeneo ya mitambo ya kurushia matangazo yaliyopo Njiro.
Alisema kila halmashauri zihakikishe zinalipa kwa wakati madeni wanayodaiwa na magazeti ya Serikali, kwani kushindwa kulipa fedha kwa wakati kunakwamisha jitihada zinazofanywa na wafanyakazi kujikwamua kiuchumi.
Alitoa rai kwa halmashauri zote nchini kutenga fedha maalumu kwa ajili ya matangazo ili kurahisisha utendaji wa kazi pamoja na kampuni kubuni mbinu za kupata matangazo na kujikwamua kiuchumi.
Mwakilishi wa Kanda ya Kaskazini upande wa Biashara wa Kampuni ya TSN, Edes Mushi alimwambia Naibu Waziri kuwa changamoto kubwa inayokabili kampuni ni ulipaji wa matangazo unaocheleweshwa na halmashauri nchini, hali inayokwamisha upatikanaji wa maendeleo na kampuni kuwa na madeni mengi yasiyolipwa kwa wakati.
chanzo;habarileo
Comments