CUF yadai baadhi ya wananchi Pemba wanakimbilia msituni.
Chamacha Wananchi (CUF) kimedai kwamba baadhi ya wanachama wake kisiwani Pemba wameanza kukimbilia msituni kutafuta upenyo wa kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini Kenya.
Chama hicho kimedai kuwa wananchi hao wanakimbia operesheni za kamatakamata zinazoendelea ikiwa ni siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Machi 20, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma, Hamad Masoud Hamad, alidai kuwa tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015, kumekuwapo na uingizwaji wa askari, vifaa na zana nzito za kivita katika visiwa vya Unguja na Pemba sambamba na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaoranda randa mitaani wakiwa na silaha za kivita.
“Sasa hivi kuna taharuki kubwa sana Pemba kutokana na vyombo vya ulinzi vilivyovamia na kuikalia Pemba na kuna makumi ya watu sasa hivi wapo maporini na wanaangalia uwezekano wa kutoroka Pemba kukimbilia Mombasa nchini Kenya. Hii inatokana na Pemba kuonekana imekaliwa kijeshi. Watu watadhalilishwa, wataumizwa, watapigwa, wanavyofikiria wao tusije tukashangaa nusu ya watu wa Pemba wakajikuta wapo huko Mombasa, Kenya,” alidai Hamad, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar.
Alisema kinachoonekana hivi sasa kitarejesha historia ya mwaka 2001 ambapo watu zaidi ya 4,000 walikimbia Pemba na kuomba hifadhi ya ukimbizi nchini Kenya baada ya kutokea machafuko yaliyotokana namatokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.
Alisema CUF inaamini matukio ya kuchomwa moto kwa maskani, matawi ya CCM, nyumba za watu na majengo ya huduma za jamii, ni muendelezo wa siasa chafu na za chuki zinazofanywa na serikali dhidi ya wananchi wasiokuwa na hatia.
“Kwa mfano, amri ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba kupiga marufuku watu kutembea baada ya saa mbili usiku na kwamba atakayevunja amri hiyo atakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la uzururaji na uzembe, ni hatua nyingine ya SMZ ya kuwahalalisha na kuwaweka wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba katika hali ngumu ya maisha,” alisema Hamad.
Alisema utendaji wa Jeshi la Polisi Zanzibar unavigawa visiwa hivyo vipande vipande.
Alidai kuwa tangu kuchomwa moto kwa matawi ya CCM na baadhi ya nyumba, wanachama wa CUF wasiopungua 30 wamekamatwa na Jeshi la Polisi na kuwekwa katika vituo mbalimbali na wengine wakinyimwa dhamana hata kwa makosa ambayo kisheria yanapaswa kudhaminiwa.
Kutokana na hali hiyo, alisema CUF imeziomba taasisi za kiraia za ndani kuacha woga na badala yake kukemea mambo yanayoendelea kujitokeza pamoja na jumuiya za kimataifa kuendelea kuitazama Zanzibar kwa umakini wa hali ya juu kufuatilia mwenendo na matukio na kuweka kumbukumbu kwa hatua za baadaye kwa kila anayeonekana kuhusika na kuonea wananchi wanyonge kwa kutumia nafasi yake ya utumishi wa umma.
“Tunatoa wito kwa Rais John Magufuli kuchukua dhamana ya uongozi, kukataa kuhadaiwa na wasaidizi wake na kukomesha matumizi mabaya ya vyombo vya ulinzi na usalama vilivyo chini ya amri yake," alisema.
Aliongeza: “Kwa hili la Zanzibar, Rais Magufuli hana pa kupenya na kwamba atawajibika kutokana na mfumo wa Katiba na sheria na utaratibu wa kuongoza nchi tuliojiwekea,” alisisitiza Hamad.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, alisema hakuna watu wanaokamatwa na kubambikiwa kesi bali wanaokamatwa ni wanaotuhumiwa na matukio ya kuchoma nyumba moto na matawi ya CCM na mahakama ndiyo itakayoamua kama wana hatia na kuwachukulia hatua za kisheria.
Alisema doria iliyoimarishwa imetokana na matukio yaliyojitokeza katika kuelekea uchaguzi mkuu ambapo kumekuwapo na matukio ya uchomaji wa moto wa nyumba, na hakuna sababu kwa wananchi kuwa na wasiwasi na doria hizo kwa kuwa zimelenga kuwatafuta wahalifu na siyo raia wema.
“Hata matawi ya CUF yalipochomwa moto kuna watu tumewatafuta na kuwakamata, na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria, sio kweli kama Polisi hatushughuliki na matukio yanayohusu CUF, kazi yetu ni kulinda usalama wa raia na mali zao bila ya kujali itikadi za vyama vyao vya siasa” alisema Kamanda Nassir.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman, alisema wananchi wanaokimbilia misituni kwa kujificha ni wale wanaotafutwa kutokana na kutuhumiwa kuhusika kwao na matukio ya kuchoma moto nyumba na matawi ya CCM katika maeneo mbalimbali ya kisiwani Pemba.
Alisema raia mwema hawezi kukimbia askari badala yake anahitaji kumpa ushirikiano, lakini alisema kwa bahati mbaya tangu kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka janakuna watu wamekuwa wakiwatisha wananchi wenzao na kufanya uharibifu mkubwa wa mali, mambo ambayo hayakubaliki katika utawala wa sheria.
chanzo;ippmedia.com/?l=89935
Comments