NOCOMPED COMMUNITY MEDIA

Pemba.

JESHI la Polisi limeanza msako wa watu waliochoma nyumba tano za wananchi wakazi wa Kangagani, ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Kituo cha Afya katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nasiri Ali, alisema katika matukio hayo hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa Polisi wala hakuna aliyejeruhiwa na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu matukio hayo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Khamis Othman alipiga marufuku mikusanyiko ya watu katika nyakati za usiku ikiwa ni sehemu ya kujaribu kupambana na kupunguza vitendo vya hujuma alivyosema vimelenga kuvuruga uchaguzi wa marudio unaotazamiwa kufanyika Machi 20 mwaka huu.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema matukio hayo yamelenga kuhujumu na kutisha wananchi ambao ni wafuasi wa chama hicho, ili wasijitokeze kupiga kura katika uchaguzi wa marudio.


Vuai aliwataka wafuasi wa CCM kuwa watulivu katika kipindi hichi kigumu na kuviachia vyombo vya dola kufanya kazi yake ya uchunguzi na kuwatia hatiani watuhumiwa wa matukio ya hujuma, ambayo hivi sasa yamekuwa yakijitokeza kwa wingi Pemba .

Comments