NOCOMPED COMMUNITY MEDIA

                                 WILAYA YA MKOANI
WANAUSHIRIKA wa kikundi cha ufugaji wa samaki kinachojulikana kwa jina la ‘Weka Heshima’ kilichopo Mwambe, Wilaya ya Mkoani, wanaiomba Serikali pamoja na wafadhili kuwasaidia vifaa vitakavyowezesha kutanua eneo la bwawa, ili waweze kuongeza uzalishaji.
Wanakikundi hao wameeleza hayo huko Mwambe wakati walipotembelewa na maafiza wa Wizara ya Mifugo na uvuvi, walipofanya ziara ya kikazi kuona matatizo na maendeleo yaliofikiwa.
Katika maelezo yao wanaushirika hao wamesema kuwa, uhaba wa eneo umekuwa ukichangia kushuka kwa uzalishaji wa samaki na hivyo kukosa maendeleo ya haraka.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Bakari hamad Haji, amesema kuwa kikundi chao kinalengo la kuongeza eneo la ufugaji, ili waweze kujipatia mahitaji ya kifamilia.
Akitaja baadhi ya vifaa vinavyohitajika katika utanuzi wa mabwawa hayo, mlezi wa ushirika huo, Hamad Shamata Hamad, amesema kuwa, ni pamoja na nyundo, mitaimbo, masururu na hata fedha zitakazoweza kuwasaidia katika mahitaji ya shughuli zao.
Kwa upande wake, mwanaushirika wa kikundi hicho, Sania Kheri Nyona, amesisitiza kupatiwa misaada kutokana na hali zao za maisha na kwamba muda wote wamekuwa wakipoteza nguvu zao katika ufugaji wa samaki , ili waweze kujikwamua na umaskini.
Nae Mkuu wa Idara ya Mipango Sera Na Utafiti Bi Asha Zahran Mohammed, amewataka wanaushirika hao kuendeleza shuguli zao pamoja na hali ngumu walionayo wakiamini kuna siku watanufaika.
Sambamba na hayo, amehimiza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu, ili kuongeza ujuzi wa ufugaji na kuahidi kuyafikisha maombi yao kunakohusika, ili yaweze kuangaliwa ni jinsi gani wanaweza kusaidiwa hali itakaporuhusu.
Kikundi cha ushirika cha ‘Weka Heshima’ kilichopo Mwambe shehia ya ‘Jombe’ kilianzishwa mwaka 2010, kikiwa na wanachama 36, wakiwemo wanaume 18 na wanawake 18, walianza shughuli za ufugaji baada ya kupatiwa utaalamu na vifaranga kutoka Idara ya mazao ya baharini Kisiwani Pemba.
MWISHO.

Comments