WILAYA YA WETE- PEMBA
OFISA Mdhamin Wizara ya Mifugo na Uvuvi Pemba, Mayasa Hamad Ali, amekabidhi mifuko ya saruji 25, yenye thamani ya shilling laki nne, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoiweka kwa wanafunzi wa kidato cha 6 katika skuli ya sekondari ya Chasasa, Wete Pemba.
Akizungumza kabla ya kukabidhi saruji hiyo, Bi Mayasa amesema kuwa, msaada huo utasaidia kwa hatua moja wapo kwa matumaini ya kuongeza madarasa ya kusomea kutokana na uhaba wa nafasi inayoikabili skuli hiyo.
Katika maelezo yake amewataka walimu hao kupokea msaada huo kwa moyo mmoja, wakiamini ndio njia moja wapo ya kupiga hatua katika ujenzi wa madarasa matatu unaoendelea kwa sasa.
Nae Mwalimu Mkuu wa skuli hiyo, Maulid Abdi Awesu, kwa niaba ya walimu wenzake pamoja na wanafunzi, aliupokea msaada huo pamoja na kutoa shukurani kwa Ofisa Mdhamin kwa kutekeleza ahadi aliyokuwa ameiweka kwa skuli hiyo.
Amesema, iwapo wahisani na wafadhili mbali mbali watajitokeza katika kusaidia ujenzi wa madarasa hayo, itachangia kwa kiasi kikumbwa upatikanaji wa nafasi ya kutosha kwa wanafunzi wanaojiendeleza na masomo skulini hapo.
Aidha, Mwalimu mkuu huyo alimtaka Ofisa Mdhamin kwa niaba ya wizara ya mifugo na uvuvi Pemba, kutofikia kikomo kwa kutoa ushirikiano wa moja kwa moja kila hali itakaporuhusu.
Skuli ya Chasasa Sekondari, imeanzishwa mwaka 2013, ikiwa na wanafunzi wapatao 876, wakiwemo wanawake 315 na wanaume 561kwa sasa ina vyumba 12 vya kusomea.
Comments