Zanzibar Kimya.
Kimya kikuu kilitawala visiwani Zanzibar jana wakati wa marudio ya Uchaguzi Mkuu huku watu wachache wakijitokeza kupiga kura.
Baadhi ya maeneo maarufu ya kibiashara ambayo kwa kawaida katika siku za kawaida huwa na mkusanyiko mkiubwa wa watu, jana ilikuwa tofauti, kwani ni watu wachache tu walionekana wakipita huku maduka karibu yote yakiwa yamefungwa.
Jumla ya vyama 14 vya kisiasa vilishiriki uchaguzi huo wa marudio.
Chama cha Wananchi (CUF) kilikwisha tangaza kuwa hakitashiriki uchaguzi huo, lakini karatasi za kupigia kura zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), zilionyesha majina ya wagombea wake wa nafasi ya Udiwani, Uwakilishi na Urais.
Hata hivyo, katika vituo vyote vya kupigia kura havikuwa na mawakala wa CUF ambao kwa kawaida hufanya kazi ya kulinda kura za wagombea wao.
Vyama vilivyoweka mawakala vilikuwa ni ADC, SAU, TLP, CCM na CCK huku vyama vingine havikuweka mawakala wao.
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya mawakala walipoulizwa wanawakilisha vyama gani, walishindwa kujibu kwa madai kwamba majina ya vyama hivyo ni magumu badala yake walinyanyua vitambulisho vyao ili mwandishi asome mwenyewe.
Wakala aliyeshindwa kutaja jina la chama anachowakilisha alikutwa katika Kituo cha kupigia kura cha Kitope jana asubuhi.
Kitambulisho cha wakala huyo kiliandikwa TLP ambacho alisema kina jina gumu na hawezi kulitamka.
WAJITIOKEZA WACHACHE
Kuhusu idadi ndogo ya wapigakura waliojitokeza, baadhi ya wasimamizi katika vituo mbalimbali vilivyowekwa Shule ya Msingi ya Kiembesamaki, walisema ilipofika saa 4:00 asubuhi, hapakuwa na watu na Nipashe ilishuhudia wakiwa wamekaa wenyewe.
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wasimamizi hao walisema mwaka jana katika uchaguzi uliofutwa, kulikuwa na idadi kubwa ya wapigakura mpaka kufikia saa 8:00 mchana, lakini jana walipungua sana.
"Mwaka jana muda kama huu saa nne asubuhi, tulikuwa hatuwezi kupumua kutokaa na idadi kubwa ya watu iliyokuwapo, lakini kama unavyoona mwenyewe kwa leo watu ni wachache mno," alisema mmoja wa wasimamizi.
Aidha, wanawake ndiyo waliojitokeza zaidi kufika katika vituo vya kupigia kura huku wanaume hususan vijana, wakionekana kwa idadi ndogo.
Baadhi ya vijana waliozungumza na Nipashe walidai kwamba watu wengi wameshindwa kujitokeza kwenda kupiga kura kwa madai kwamba hawawezi kufanya uchaguzi mara mbili.
Abdul Makame, mkazi wa Mbweni alisema uchaguzi huru na wa haki uliishafanyika mwaka jana na kwamba wao hawatambui kinachofanyika kwa sasa.
Hadija Bakari mkazi wa Kiembesamaki, alisema wanawake wamejitokeza kwa wingi kuliko wanaume kwa kuwa uchaguzi huo wanaume wao walionywa wasiwazuie kwenda kupiga kura kama walivyofanya mwaka jana.
Aidha, badhi ya wananchi katika mitaa mbalimbali ya Zanzibar, walionekana wakiendelea na kazi zao kama kawaida badala ya kwenda kupiga kura kama inavyokuwa kila unapofanyika Uchaguzi Mkuu.
ULINZI WAIMARISHWA
Jana asubuhi kulikuwa na ulinzi mkali katika maeneo ya kupigiakura, mitaani ingawa baadaye askari wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, walionekana kama hawakuwa na kazi ya kufanya kwa kuwa wananchi waliojitokeza walikuwa wachache na wengi wao walionekana kufuata taratibu zikiwamo za kukaa katika mstari.
chanzo;ippmedia.com
Comments