Muasisi wa Mapinduzi Zanzibar aaga dunia
MMOJA wa waasisi 14 wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964, Hamid Ameir amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.
Alifikwa na umauti jana asubuhi na kuzikwa leo kijijini kwake Donge Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa heshima zote za chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Kifo cha Ameir kimethibitishwa na upande wa ndugu, chama na serikali, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema Ameir atakumbukwa daima kwa mchango wake ambapo baada ya mapinduzi alifanya kazi bega kwa bega na viongozi wenzake kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kutekeleza na kutimiza malengo yaliyoasisiwa katika Ilani ya chama kilichopigania uhuru, Afro Shiraz (ASP).
ASP baadaye kiliungana na TANU na kuzaliwa rasmi kwa CCM Februari 5, mwaka 1977.
Ameir, alishiriki kikamilifu katika Mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa Sultani wa Oman na wazalendo walio wengi kushika hatamu ya kuongoza dola chini ya kiongozi wao, Rais Abeid Amaan Karume.
Usultani ulidumu Zanzibar tangu mwaka 1856 chini ya Sultani Sayyid Said hadi mwaka 1964, chini ya Sultani Jamshid bin Abdullah. Jumla ya masultani 11 walitawala Zanzibar katika kipindi hicho.
Hadi anafikwa na umauti, Ameir alikuwa akiamini Mapinduzi ndiyo yaliyomkomboa mwananchi wa Zanzibar na wazalendo walio wengi kushika hatamu ya kuongoza nchi na pia kunufaika na fursa mbalimbali, zikiwemo za elimu na umiliki wa ardhi.
Mwandishi wa gazeti hili ambaye alifanya mahojiano ya mwisho na Ameir katika matayarisho ya makala kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari mwaka huu nyumbani kwake Mtoni, alisema anajivunia mapinduzi hayo kwa sababu yaliwafanya wananchi kuwa huru katika nchi yao baada ya kuwa chini ya utawala wa kigeni kwa miaka mingi.
Katika mahojiano hayo, aliwaasa vijana kamwe wasijaribu kuyabeza na kuyadharau Mapinduzi ya Januari 12, 1964 kwani kabla ya tukio hilo wananchi hawakuwa na uwezo na fursa za kumiliki ardhi kwa ajili ya makazi ya kudumu na kilimo, matibabu pamoja na elimu ambayo ilikuwa ikitolewa kwa njia ya matabaka.
Kwa upande wa CCM Zanzibar, chama hicho kimeelezea kusikitishwa na kifo cha muasisi huyo, aliyetajwa kuwa kiongozi shupavu aliyefanya kazi kwa maslahi ya taifa lake na kushiriki kikamilifu hadi kufanikisha mapinduzi yanayonufaisha wengi.
Ameir alishika nafasi mbalimbali baada ya mapinduzi ya Zanzibar akiwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Bodi mbalimbali za SMZ.
chanzo;http://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/7339-muasisi-wa-mapinduzi-zanzibar-aaga-dunia
Comments