Mbaroni kwa kuchoma ofisi za CCM Zanzibar.
Jeshi la Polisi Zanzibar limewakamata watu 31 kwa tuhuma za kuchoma moto Nyumba, matawi ya CCM na majengo ya huduma za jamii pamoja na waliomzomea Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kisiwani Pemba.
Watu hao wamekamatwa kutokana na msako mkali unaoendelea katika mikoa miwili kisiwani humo tangu miundombinu hiyo, kuhujumiwa kwa kuchomwa moto kwa sababu zinazodaiwa kuwa za kisiasa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, alisema jana kuwa watu 20 wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na matukio uchomaji moto majengo.
Alisema pamoja na kukamatwa kwa watu hao, polisi wanaendelea kuimarisha ulinzi wa doria wa kuwasaka watu wengine na kuchunguza chanzo cha hujuma hizo.
Matukio ya kuchomwa moto nyumba, matawi ya CCM na majengo ya huduma za jamii, yametokea huku Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, akiendelea na ziara ya kikazi kisiwani Pemba.
Majengo yaliyochomwa moto yamefikia 15, zikiwamo Ofisi za CCM katika matawi ya Tibrinzi, Kipapo, Shidi Mkanyageni, Muambe na Kendwa.
Majengo mengine yaliyochomwa moto ni maskani ya CCM Gando, nyumba za CCM Makangale na Msuka, ofisi ya kikundi cha ushirika wa Usumba, Kituo cha Afya Kiuyu Minugwini, na nyumba tano zilizochomwa moto katika maeneo ya Kangagani, Mgeni Nje Tumbe, na Kojifer kisiwani humo.
Watu hao walikamatwa katika Kijiji cha Mpopooni, wilaya ya Micheweni na kufikishwa katika kituo cha Polisi Micheweni wakiwa chni ya ulinzi.
Watu hao Omar Hassan Hamad(42) Hassan Omar Hassan (16) Hassan Nassor Hassan (12) na Hamad Nassor Hassan (11), wote ni wakazi wa kijiji cha Mpopooni.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo Hassan Nassir alisema hana taarifa za mpaka jana za kukamatwa kwa watu hao.
Tangu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kufuta matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 28, mwaka jana, kumeibuka mgawanyiko mkubwa wa watu wanaounga mkono uchaguzi kurudiwa na wanaopiga na kusababisha matukio ya uchomaji moto kujitokeza kisiwani humo.
chanzo;http://www.ippmedia.com/frontend/?l=89902
Comments