Mama Magufuli awakabidhi msaada wazee, wasiojiweza.

Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli, amewakabidhi msaada wazee walemavu na wasiojiweza wa kituo cha Bukumbi kilichoko kata ya Idetemya, Misungwi, uliotolewa na benki ya CRDB wenye thamani ya Sh. milioni 53.

Msaada huo uliotolewa jana kituoni hapo, ikiwa mara ya kwanza kwa Mama Janeth tangu alipoombwa kuwa mlezi wa kituo hicho.

Walemavu na wasiojiweza hao 108 wa kituo hicho, walikabidhiwa mchele, unga, maharage, sukari na mafuta ya kula na nishati ya umeme wa jua.

Akizungumza baada ya kukaribishwa na Ofisa Mfawidhi wa kituo hicho, Michael Bundala, Mama Janeth aliishukuru CRDB kwa  kutoa msaada katika kituo hicho.

Aliwataka wahisani mbalimbali yakiwamo mashirika, wadau na taasisi kuwasaidia wazee hao na kutatua changamoto zinazoikabili kambi hiyo na zyingine za wazee na wasiojiweza.

“Nimetembelea kambi 17 za wazee nchini, wana changamoto nyingi sana ila nitajitahidi kwa kadri niwezavyo kushirikiana na wadau mbalimbali kuwasaidia wazee wetu,” alisema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei, alisema msaada huo ni moja ya malengo ya benki hiyo kuhakikisha inatoa fungu la mapato yake kwa watu wenye uhitaji, wakiwamo walemavu na wazee.

Dk. Kimei alisema msaada huo ni shukrani kwao kwa kuadhimisha miaka 20 ya utoaji wa huduma nchini na kuwa na amana Sh. trilioni 5.5 wakati mkoa wa Mwanza pekee ikiwa na amana ya Sh. bilioni 500, huku wakiwa na matawi 50 kwa mikoa ya kanda ya ziwa kutoka matawi matatu.

“Japo tumechelewa lakini tutajitahidi kuwasaidia watu wenye changamoto mbalimbali wakiwamo wazee, walemavu na wasiojiweza, hivyo tutaanza kulenga misaada yetu kwenye vituo vya wasiojiweza ili kufaidisha wengi zaidi,” alisema.

CRDB ilitoa msaada wa tani sita za mchele, unga wa mahindi (tani sita), maharage (tani tatu), lita 1,000 za mafuta ya kula, sukari tani mbili na nusu pamoja na umeme wa jua ambavyo vyote viligharimu Sh. milioni 53.

Bundala alisema kituo hicho kilianzishwa na serikali  kusaidia kutoa matunzo kwa kundi maalumu la wazee na walemavu wanaotoka mikoa ya kanda ya ziwa, mwaka 1974.

Alisema kwa sasa kituo hicho kinahudumia wazee 108 wakiwamo wanaume 36, wanawake 55 na watoto 17 ambao wako chini ya miaka 18.

Aidha, Mfuko wa Pensheni (PPF), ulitoa msaada wa mashine ya kufulia ambayo iliyokabidhiwa kwa Mama Janeth toka meneja wa mfuko huo kanda ya ziwa, Meshack Bandawe, huku jumuiya ya misikiti ya Wahindu wakitoa msaada wa vyakula vyenye thamani ya Sh. milioni 3.5.

chanzo;http://www.ippmedia.com/?l=89662

Comments