Magufuli: Tusibaguane kwa itikadi za dini, vyama.

Rais Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania wasibaguane kwa itikadi za kidini ama vyama, huku akiwawaomba wasichoke kuendelea kumuombea kwa kuwa jukumu la uongozi ni gumu, zito na msalaba mzito.
 
Amesema bila maombi hawezi kufanikisha kuifikisha Tanzania katika maendeleo makubwa.
 
Rais Magufuli aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waumini wa Kanisa Kuu la Kilutheri la Azania Front jijini Dar es Salaam jana wakati akiwasilisha salamu zake za Pasaka.
 
Alisema katika maadhimisho ya kufufuka kwa Bwana Yesu Kiristo, anatakiwa afufuke na Watanzania katika matendo, kutanguliza upendo na kushirikiana. 
 
“Nawashukuru sana kwa jinsi mnavyoendelea kuniombea, naomba msichoke ili nitimize yote si kwa mapenzi yangu, lakini kwa ajili ya Watanzania na Mwenyezi Mungu,”  alisema Dk. Magufuli huku akisema ameshiriki ibada hiyo kama Mkristo wa kawaida.
 
“Yesu alipokuja duniani, hakubagua makabila yetu, hakubagua dini zetu, hakubagua imani zetu, alitufia sote kwa sababu lengo kubwa lilikuwa ni kutupatanisha na Mungu. Wakati tukifuata mafundisho hayo, Watanzania tusibaguane katika vyama vyetu, dini wala makabila, tuwe wamoja kumtumikia Mungu wetu na katika umoja wetu tutafanikiwa kuifanya Tanzania yenye neema,” alisema.
 
Aidha, aliwataka Watanzania kufufuka na Kristo kwa kufanya kazi kwa bidii, kwa sababu katika maandiko imeandikwa asiyefanya kazi na asile.
 
"Kila mmoja akifanya kazi, nchi haitahitaji wala kubembeleza misaada ya masharti kutoka nje kwa kuwa ni yenye neema, ina kila kitu na ikisimama imara na kila mmoja akatimiza wajibu wake, itakuwa ni nchi inayotoa msaada kwa nchi nyingine duniani," alisema.
 
Dk. Magufuli ambaye alisema hakutoa taarifa za ujio wake kwenye ibada hiyo na ni mara yake ya nne kusali kanisani hapo, alisema nyakati za usiku alikuta ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kutoka kwa Mkuu wa KKKT nchini, Askofu Dk. Frederick Shoo, akimtakia heri ya Pasaka, ambao ulimfariji sana.
 
Baada ya salamu hizo, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa na waumini, walifanya maombi maalum kwa ajili ya Rais Magufuli na familia yake ili kumwezesha kutekeleza majukumu ya kitaifa.
 
“…Mungu mtumishi wako (Magufuli), mara kadhaa ameomba tumwombee kwa njia ya Yesu. Tumeona na kusikia imani ya mtu ndiyo inayomwokoa, endelea kukutana naye… asante Mungu kwa kutupa kiongozi ambaye anakutamka wewe (Mungu), tena anaomba hadharani kwamba tuendelee kumwombea,” hiyo ni sehemu ya maombi hayo.
 
MALASUSA: TUKIWATAJA WALA RUSHWA HAITAKUWAPO
Awali, katika mahuburi yake, Dk. Malasusa ambaye alikuwa Mkuu wa Kanisa hilo nchini kwa vipindi viwili mfululizo hadi mapema mwaka huu,  aliwataka waumini kutimiza wajibu wao katika kusaidia utekelezaji wa shughuli za serikali ikiwamo kupinga rushwa ambayo imekithiri huku waumini wakiwa katika kundi la walalamikaji.
 
“Tunalalamika miaka na miaka juu ya rushwa, kama Ukristo upo kwa nini rushwa, mauaji ya albino na vikogwe yaendelee kuwapo, hivi tukiamua wote kuwataja wanaopokea rushwa hatuwezi kumaliza hili tatizo? Mimi nikiwajua nawataja hadharani. Tunaogopa kwa kuwa hatujasimama sawa sawa,” alisema.
 
Aidha, alisema serikali ya awamu ya tano inaleta matumaini makubwa kwa Watanzania na kwamba ni wakati wa kila mmoja kutimiza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kumuomba Mungu roho ya ujasiri na kusimamia mambo.
 
Dk. Malasusa alisema ufufuko wa Kristo uwakumbushe waumini na kuwajaza roho ya upendo na kupendana hatua itakayoondoa mauaji na dhuluma.
 
“Tunamshukuru Mungu kwa kutupa kiongozi anayependa ibada, nawashangaa viongozi mbalimbali ambao hawapendi ibada wala hawana hofu ya Mungu, ukikuta kiongozi anaongoza watu na hana hofu ya Mungu na anaowaongoza ni watu wa Mungu, ogopa kuongozwa na mtu kama huyo,” alisisitiza.
 
Aidha, alimuomba Mungu kugusa mioyo ya viongozi wa ngazi mbalimbali nchini kutamani moyo wa ibada, kutenda mema na kwamba iwapo neno lingehubiriwa na kufuatwa ipasavyo, hata bajeti ya magereza ingepungua.
 
Askofu Dk. Malasusa aliwaomba waumini kujenga upendo wa kifamilia na malezi bora ya familia na kueleza kuwa kwa sasa kuna mfarakano mkubwa kwenye ndoa ambazo zimesababisha watoto kulelewa katika maadili yasiyofaa tofauti na zamani ambapo walilelewa ndani ya familia zenye hofu ya Mungu.
 
“Rais wetu ni mtu wa wote, amedhihirisha hilo kwa kushiriki nasi kwenye ibada hii, nilipopewa taarifa na wasaidizi wake sikuamini, nilifikiri wamekosea kuleta taarifa husika, lakini kumbe ni kweli na ameshiriki nasi katika Ibada hii ya Ufufuko,” alisema Askofu Malasusa.
chanzo;ippmedia.

Comments