CUF yaibua hofu Baraza la Wawakilishi.

Hofu ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupungua kasi ya kusimamia serikali, imeanza kujitokeza baada ya wapinzani kususia uchaguzi wa marudio na kusababisha baraza hilo kuundwa na CCM pekee.
 
Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya Wawakilishi katika ukumbi wa Baraza hilo, Chukwani mjini hapa, walisema jana kuwa upinzani una umuhimu katika kuharakisha maendeleo kwa kuisimamia serikali kutekeleza majukumu yake, ikiwamo kutatua kero za wananchi.
 
“Wapinzani walikuwa na uhuru mkubwa wa kukosoa serikali na kufichua vitendo vya ufisadia na matumizi mabaya ya madaraka, sote tunakumbuka,” alisema mjuumbe mmoja wa Viti Maalum visiwani hapa.
 
Mwakilishi huyo kutoka kisiwani Pemba alisema kambi ya upinzani ndiyo injini ya kujenga misingi ya utawala bora katika kusimamia uwajibikaji na kupinga vita ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
 
Hata hivyo, Mwakilishi wa Viti Maalum, Panya Ali Abdalla, alisema jambo la msingi ni Baraza kuwa katika umoja na wajumbe ambao watakosa nafasi ya uwaziri, waisimamie serikali kwa kuweka mbele maslahi ya nchi na wananchi wake.
 
Alisema Rais wa Zanzibar (Dk. Ali Mohamed Shein), bado nafasi ya kuchagua wapinzani kupitia nafasi zake kumi ili kujenga umoja na kuendeleza msingi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
 
“Viongozi wa upinzani walioshiriki uchaguzi wapo na rais bado ana uwezo wa kutumia nafasi zake 10 kuwateua na kuendeleza msingi wa serikali ya umoja wa kitaifa,” alisema Panya.
 
Mwakilishi wa Kwahani, Ali Salum Haji, alisema ni jambo la faraja kuona wawakilishi wengi waliofanikiwa kuingia katika chombo hicho, wengi wakiwa wapya na wanaweza kuonyesha mabadiliko makubwa ya utendaji katika baraza hilo.
 
Alisema jambo la msingi viongozi watakaonufaika na uteuzi wa nafasi za uwaziri na watendaji wakuu lazima wawe wenye sifa, uwezo na suala la umri na elimu vipewe nafasi.
 
“Tumeona rais ameonyesha uadilifu mkubwa katika kipindi cha uongozi wake. Lazima wapatikane watu imara wenye sifa kama mwenyewe ili kufanikisha malengo ya serikali ya kuwapatia maisha bora wananchi,” alisema.
 
Hata hivyo, alisema suala la vijana kupewa nafasi za uongozi ni jambo muhimu ili serikali iweze kutumia nguvu zao na taaluma zao katika kuharakisha maendeleo ya Zanzibar.
 
“Tunahitaji serikali yenye viongozi na watendaji wenye uwezo, elimu na uzoefu ili kufikia kasi ya maendeleo kama inavyojitokeza Tanzania Bara,” alisema.
 
Sambamba na hilo, alisema kuna umuhimu wa kutumia nguvu kazi ya vijana na wasomi katika kuunda serikali ili kuharakisha maendeleo ya Zanzibar pamoja na kutatua kero za wananchi kwa wakati muafaka.
 
Alisema kuwa kama mambo hayo yatazigatiwa, serikali itaweza kutekeleza majukumu yake bila wasiwasi, ikiwamo utekelezaji wa ilani.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu, Haji Omar Kheir, alisema hakuna athari zozote kukosekana wapinzani ndani ya baraza hilo kama wawakilishi watafanya kazi kwa umakini katika kusimamia utekelezaji wa ilani ya chama chao.
 
Waziri huyo wa zamani wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ alisema wajumbe wa Baraza, pamoja na kuwa wote wanatoka CCM, wana huru wa kukosoa na kuisimamia serikali katika utekelezaji wa majukumu.
 
Wakati hayo yakitokea, baadhi ya wananchi katika Manispaa ya Zanzibar walisema kunahitajika sura mpya katika Baraza la Mawaziri na watendaji ili kuongeza kasi ya uwajibikaji kutokana na wengi wao waliomaliza muda kuwa wazee.
 
Said Juma Khatib, mkazi wa Mbweni, alisema Baraza la Mawaziri lililomaliza muda wake baadhi ya mawaziri wake walikuwa mzigo na wengine wakiwa katika nyadhifa hizo kwa Zaidi ya miaka 20, huku watendaji waliositaafu kwa mujibu wa sheria wakiogezewa mikataba ya kazi.
 
Mohamed Mussa Said, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tunguu alisema  utaratibu wa watendaji wakuu wastaafu kuongezewa mikataba ya kazi imekuwa kero kubwa wakati vijana wasomi wakibakia vijiweni bila ajira.
chanzo;ippmedia.

Comments