Spika
wa Bunge, Job Ndugai leo Jumanne Juni Mosi, 2021 amemtoa katika
ukumbi wa Bunge mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichwale kutokana na
kuvaa suruali iliyombana.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, wabunge wanawake hawaruhusiwi kuvaa suruali za kubana.
Mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, alisimama mbunge wa Nyang'wale (CCM), Hussein Amar na kuomba mwongozo wa Spika.
"Spika
nasimama kwa kanuni ya 70 inayohusu mavazi ya staha kwa wabunge,
kanuni imeeleza wazi kuhusu mavazi hayo na kwa akina dada lakini humu
ndani kuna wabunge wamevaa nguo ambazo hazina staha," amesema Amar.
Spika Ndugai alimpa nafasi mbunge huyo kumtaja mwenzake aliyevaa mavazi ambayo hayakuwa na staha ili iwe mfano.
"Mbunge
huyo yuko hapo katika mkono wangu wa kulia, amevalia tisheti lakini
naomba umuite mbele uone suruali aliyovaa namna ilivyobana, amevaa
miwani," amesema Ameir bila kumtaja jina.
Spika alisimama na
kumtaka mbunge aliyevaa mavazi hayo asimame na aondoke ndani ya ukumbi
ili akavae mavazi yenye staha ndipo atarejea tena bungeni.
Sichwale alisimama akabeba mkoba wake na kutoka nje ya ukumbi wa Bunge.
Spika
Ndugai ameagiza askari wote katika milango ya kuingia bungeni wawe
makini wasiruhusu wabunge kuingia wakiwa wamevaa mavazi yaliyokatazwa.
Comments