Waziri wa Elimu Zanzibar :‘Tuition’ zinawachanganya wanafunzi.

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, amewataka wanafunzi kuacha tabia ya kuhangaika kutafuta masomo ya ziada (tuition) badala yeke wazingatie zaidi masomo wanayofundishwa na walimu wao darasani.
Alitoa witi huo katika kikao cha kujadili na kutathmini changamoto za elimu hasa katika skuli ambazo zimefanya vibaya katika matokeo ya kidato cha sita ambazo ni Tumekuja na Haile Sellasie,kikao kilichowashirikisha Mbunge na Mwakishi wa jimbo la Kikwajuni na  wadau wa elimu.
“Wanafunzi wamekuwa wakiranda njiani kutafuta ‘tuition’ wakiamini kuwa zitawasaidia katika masomo yao jambo ambalo sio kweli kwani ‘tuition’ nyingi zipo kimasilahi ya walimu  na sio kwa faida ya wanafunzi,” alisema.
Aidha aliwataka wanafunzi hao kuamini zaidi masomo ambayo wanafundishwa na walimu wao madarasani, kwani walimu wengi wa ‘tuition’ hawana taaluma ya ualimu na hawajui wanafunzi wanataka nini na badala yake huwafundisha vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wao.
“Jambo hili linasababisha kufeli kwa wanafunzi wengi kwani hawaingii madarasani mpaka kipindi cha mitihani hivyo nawataka wanafunzi kuhudhuria katika vipindi vya darasani,” alisema.
Aidha aliwataka wanafunzi kushirikiana na kusaidiana katika masomo yao kwani wapo ambao wana uwezo na wengine uwezo wao mdogo hivyo wakishirikiana itasaidia kupata ufaulu mzuri.
Pamoja na hayo, aliwaomba  wazazi, walimu, wanafunzi pamoja serikali kushirikiana kuhakikisha wanafunzi wanapata ufaulu mzuri na sio kuwaachia jukumu walimu peke yao.
Mapema Mbunge wa jimbo la Kikwajuni, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Hamad Yusuf Masauni, alisema dhamira ya kikao hicho ni kujadili na kujua changamoto zilizosababisha  kushuka kwa ufaulu wa mitihani katika skuli ya Haile Sellasie pamoja na Tumekuja.
“Tumeona kuna kasoro mwaka huu katika skuli zetu hizi mbili za jimboni kutokea katika skuli 10 za mwisho jambo ambalo sio la kawaida na ndio maana tumeitana hapa kujadili changamoto zinazowakabili,” alisema.
Aidha aliwaomba walimu waimarishe mazingira ya kusomea wanafunzi pamoja na kuanzisha utaratibu wa masomo ya ziada ili kupunguza wimbi kubwa la wanafunzi wanaokwenda kutafuta ‘tuition’ nje ambazo nyingi zipo kwa maslahi zaidi.
Aidha aliwaahidi walimu na wanafunzi wa skuli zilizopo katika jimbo lake ambao watafanikiwa kufanya vizuri katika masomo yao,watapata motisha ya kuendelea kufanya vizuri zaidi.
Kwa upande wake, Mwalimu wa skuli ya Tumekuja, Hassan Ame, alisema, changamoto inayowakabili ni idadi kubwa ya wanafunzi ikilinganisha na madarasa yaliyopo.
Aidha alisema, changamoto nyengine ni wanafunzi ambao wapo kidato cha tano na sita kutokuwa na imani na walimu wao hivyo wengi wao hutafuta zaidi ‘tuition’ za nje kuliko kumtegemea mwalimu.
Nae Mwalimu kutoka skuli ya Haile Sellasie, Tatu Ameir, alisema changamoto kubwa inayowakabili ni upungufu wa madarasa.
Zanzibarleo.

Comments