Wanazuoni wa Kiislamu Yemen waikosoa Saudia kwa kutumia vibaya ibada ya Hija.

Wanazuoni wa Kiislamu Yemen waikosoa Saudia kwa kutumia vibaya ibada ya Hija
Jumuiya ya Wanazuoni wa Kiislamu nchini Yemen imetangaza kuwa, mienendo ya utawala wa kifalme wa Saudi Arabia ya kuitumia vibaya ibada ya Hija kwa malengo yake ya kisiasa ni balaa na maafa kwa matukufu ya Kiislamu.



Taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Maulama wa Yemen pia imesema kuwa kuwapo kambi za kijeshi za Marekani na Uingereza huko Saudi Arabia ni hatari kubwa kwa maeneo matakatifu ya Makka na Madina. 
Saudi Arabia imekuwa ikikosolewa na kulaumiwa mara kwa mara kutokana na mienendo yake ya kusimamia vibaya ibada ya Hija kwa kutegemea maslahi yake ya kisiasa. 
Kwa msingi huo Kamati ya Kimataifa ya nchi za Kiislamu miaka kadhaa iliyopita ilitoa pendekezo la kutaka amali za ibada ya Hija zisimamiwe na kamati maalumu ya kimataifa ya Ulimwengu wa Kiislamu lakini pendekezo hilo limepingwa na viongozi wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia. 
Miito mingi zaidi ya kutaka Hija isimamiwe na kamati ya kimataifa ya nchi za Kiislamu imetolewa baada ya mamlaka za utawala wa Aal Saud kukwamisha uingiaji, usafirishaji na utoaji hudumu za makazi kwa mahujaji kutoka Qatar na Yemen na vilevile kutokana na vizuizi walivyowekewa mahujaji kutoka Iran na Libya. 
Kwa mfano tu mwaka jana, ikiwa ni katika hatua yake ya kutaka kupata ridhaa ya utawala haramu wa Israel na Marekani, utawala wa Saudi Arabia uliwanyima maelfu ya Wapalestina vibali vya kuingia nchini humo kwa ajili ya kufanya ibada ya Hija. 
Kutokana na hatua hiyo ya Saudia ambayo ilitekelezwa kwa ushirikiano na Israel, Wapalestina waliotaka kwenda Hija huko Saudi Arabia kutokea Jordan, Lebanon, Quds Mashariki na ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu  walinyimwa vibali vya kuingia nchini humo.
parstoday.

Comments