Umoja wa Mataifa: Israel ni miongoni wanaoliuzia silaha jeshi la Myanmar.

Umoja wa Mataifa: Israel ni miongoni wanaoliuzia silaha jeshi la Myanmar
Utawala haramu wa Israel umetajwa kuwa miongoni mwa tawala saba duniani zinazoliuzia silaha jeshi la Myanmar ambalo limekuwa likishirikiana na mabudha wenye misimamo mikali wa nchi hiyo kuwaua kinyama Waislamu wa jamii ya Rohingya.


Hayo yamo katika ripoti ya Umoja wa Mataifa ambayo imeeleza kwamba, kwa akali mashirika 15 kutoka mataifa mbalimbali ukiwemo utawala ghasibu wa Israel yamekuwa yakiliuzia silaha jeshi la Myanmar kuanzia 2016.
Nchi nyingine zilizotajwa katika ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ambazo zimekuwa zikiliuzia silaha jeshi la Myanmar ni Russia, China, Korea Kaskazini, Ufilipino, Ukraine na Singapore. 
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kususiwa makampuni yote ya Myanmar ambayo yanashirikiana na jeshi la nchi hiyo ambalo linatuhumiwa kutenda jinai dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wa jimbo la magharibi mwa nchi hiyo la Rakhine.
Hivi karibuni pia timu ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa ilizitaka nchi za dunia kusitisha miamala ya kifedha na jeshi la Myanmar linaloendelea kuua Waislamu wa jamii ya Rohingya katika mkoa wa Rakhine.
Itakumbukwa kuwa, jeshi hilo kwa kushirikiana na Mabudha wenye misimamo ya kigaidi lilifanya mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, miaka miwili iliyopita katika jimbo hilo la Rakhine.
Katika hujuma hizo jeshi hilo liliua karibu Waislamu elfu saba wa jamii ya Rohingya na kuwajeruhiwa wengine elfu nane, huku wengine zaidi ya milioni moja wakilazimika kuwa wakimbizi nje ya nchi hiyo.
parstoday.

Comments