Umoja na VIjana wa CCM watakiwa Kufkiria kuwa na maskani Kujifunzia.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Balozi Seif Ali Iddi, ameuomba Umoja wa Vijana wa CCM, kufikiria kuwa na maskani za IT ambazo vijana wengi watapata fursa ya kujifunza.
Alitoa kauli hiyo katika usiku wa vijana wa mkoa mjini magharibi uliojumuisha uzinduzi wa mfumo wa usajili wa wanachama wa umoja huo kwa njia ya kielektroniki na tovuti, katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni.
Alisema walimu wa kompyuta lazima waanze kuwatayarisha vijana ili wawe na uwezo wa kushindana na wenzao kutoka mataifa mbali mbali duniani.
Alisema kwamba vijana lazima wabadilike kwa mujibu wa mazingira ambapo kazi kubwa iliyo mbele yao ni kujipanga  kuwa wajuzi  vyenginevyo wataachwa nyuma.
Alisema ametiwa moyo na uongozi wa UVCCM kuliona jambo hilo, lakini pamoja na jambo zuri walilolifanya alitahadharisha kwamba kuwa na mfumo wa kisasa wa usajili wa wanachama hakumaanishi UVCCM itakuwa na wanachama wengi zaidi.
Alieleza kwamba mfumo huo kazi yake ni kurahisisha usajili, lakini kazi ya kutafuta wanachama wapya wa kujiunga na umoja huo bado ipo pale pale.
Aliwaeleza vijana hao kwamba kazi kubwa iliyo mbele yao ni kuwashawishi vijana kujiunga na umoja huo ili kuhakikisha CCM inashinda katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Akizungumzia uwekaji wa taarifa kwenye tovuti, aliwatahadharisha vijana hao kuelewa kwamba jumuiya nyingi hapa nchini zikiwemo taasisi za serikali zimefungua tovuti lakini lakini taarifa nyingi zimepitwa na wakati.
“Tovuti yenu inatakiwa ipigie debe jumuiya yenu na Chama cha Mapinduzi na wala isitumike kuwapigia debe Viongozi wenu kwa ajili ya kujipatia vyeo,” alisema.
Aliwataka viongozo wa umoja huo kuhakikisha vijana wao ni wazuri kitaaluma hasa katika eneo la propaganda kwa ajili ya kujibu hoja za wapinzani na kukisaidia chama chao kuendeleza ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mapema Mwenyekiti wa kamati ya elimu, habari na michezo UVCCM mkoa magharibi, Abdullah Ramadhan Abdullah, alisema mfumo wa usajili wa wanachama kielektroniki na tovuti utakuwa ukibadilishwa kulingana na mahitaji.
Alisema mafunzo yametolewa kwa vijana 10 watakaotoa elimu itakayomuwezesha mwanachama kuwa na uwezo wa kujiingia taarifa zake katika kompyuta.
Hata hivyo, alifahamisha kwamba mafunzo kwa vijana yataendelea kutolewa katika ngazi ya wilaya, jimbo hadi wadi ambapo wahusika watakuwa na fursa za kutuma taarifa na matukio kwa kutumia Facebook, twitter na instagram.
Alisema hatua hiyo itakwenda sambamba na maandalizi ya kuanzishwa kwa TV Online itakayofuatiwa na utayarishaji wa vipindi na kuviingiza kwenye televisheni hiyo.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua mfumo huo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Abdalla Juma Saadala,aliipongeza jumuiya hiyo  kwa kubuni mbinu za kuwafuata vijana katika maeneo yao kujiunga na umoja huo.
Zanzibarleo.

Comments