Skuli 20 za mwisho zilizo feli MOCK zijieleze.

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud, ametoa wiki mbili kwa walimu wakuu wa skuli za mkoa huo zilizoshika nafasi 20 za mwisho katika mitihani ya majaribio kubainisha sababu za matokeo hayo.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya matokeo ya mitihani hiyo iliyofanyika mwezi uliopita, Ayoub alisema kufanya hivyo kutasaidia kujipanga vyema kwa ajili ya mitihani ya mwisho wa mwaka.
Alisema kwa ujumla matokeo ya mitihani hiyo ni mazuri ila skuli zilizotokea mwisho zinapaswa kueleza sababu na mikakati waliyonayo kujinasua katika nafasi hizo ili kwenda sambamba na dhamira ya mkoa huo ya kuimarisha ubora wa elimu.
“Hatuwezi kuacha sababu zilizotajwa hapa kuharibu ubora wa matokeo haya, lazima wenzetu hawa watuambie ilikuwaje na namna gani tutatoka hapo ili maelezo yao yaisadie kamati ya maendeleo ya elimu ya mkoa”, alisema Ayoub na kusisitiza kuwa agizo hilo linahusu na skuli binafsi.
Alieleza kuwa wakati serikali ikiendelea na jitihada za kuimarisha miundombinu katika sekta ya elimu, wadau wengine wakiwemo wazazi wanapaswa kutimiza wajibu wao kikamilifu.
“Kwa idadi ya wanafunzi ambao hawajafanya mitihani kutokana na utoro, wazazi lazima tuwajibike kwa elimu ya watoto wetu kwani hii ni hasara kwa serikali ambayo inagharamia mitihani baada ya kuondoa michango katika ngazi ya elimu ya msingi na sekondari,” alisema.
Akiwasilisha matokeo hayo mbele ya Mkuu huyo wa mkoa, Mwenyekiti wa Kamati ya mitihani hiyo mwalimu Mussa Hassan Mussa, alisema kuna ongezeko la ufaulu kwa asili 2.22 kwa matokeo ya mitihani ya mwaka uliopita sambamba na ongezeko la watahiniwa.
“Katika mwaka 2018 idadi ya watahiniwa ilikuwa 8,774 na 5,449 sawa na 63.20 walifaulu ambapo kwa mwaka huu waliofanya mitihaqni walikuwa 13,436 na 8,622 sawa na asilimia 65.42 walifaulu,” alifafanua.
Aidha alizitaja skuli 10 zenye wanafunzi zaidi ya 45 zilizofanya vizuri katika mitihani hiyo kuwa ni Lumumba, Dole Mikindani, SOS, Al-Ihsan, Kiponda, Suni Madrasa, Francis Maria, Trifonia, Tumekuja na Lurent wakati zenye wanafunzi chini ya 45 ni Brilliant Academy, Zanzibar Progressive, FEZA Zanzibar na Munaa Academy.
Nyengine ni St. Monica, Al-Mubarak, Juma Islamic, Stone Town na Sufaa wakati skuli 10 zilizofanya vibaya ni Ndame Academy, Sun City, Regezamwendo, Nyerere, Kisauni, Forodhani, Chuini, Kombeni, Mtoni Kigomeni na Mwenge kwa skuli zenye watahiniwa 45 na zaidi.
Akizungumzia matokeo hayo, Mwenyekiti wa bodi ya elimu ya mkoa huo, Mabrouk Jabu, alipongeza juhudi za wadau wote wa elimu waliofanikisha mitihani hiyo na kuwataka kuitumia kama kipimo kwa mitihani ya mwisho wa mwaka.
“Matokeo haya yanatoa picha ya namna gani ya kukabiliana na matokeo ya mwisho wa mwaka hivyo walioanguka wafanye juhudi kuinuka na waliosimama waendelee kukaza kamba,” alisema.
Zanzibarleo.

Comments