India yatayarisha mazingira ya kulitwaa kikamilifu eneo la Kashmir.

India yatayarisha mazingira ya kulitwaa kikamilifu eneo la Kashmir
Serikali ya India imefuta sheria inayolipa hali makhsusi eneo la Kashmir linalozozaniwa baina ya nchi hiyo na Pakistan katika jitihada za kuliunganisha kikamilifu na ardhi ya India.


Hatua hiyo inahesabiwa kuwa harakati kubwa zaidi inayochukuliwa na India ya kulitwaa kikamilifu eneo hilo lenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu tangu miaka 70 iliyopita.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa India Amit Shah ameliambia Bunge la nchi hiyo kwamba, serikali kuu itafuta kifungu nambari 370 cha Katiba kinacholipatia eneo linalogombaniwa la Kashmir hali makhsusi inayoliruhusu eneo hilo kutunga sheria zake makhsusi.
Amit Shah ameongeza kuwa, Katiba ya India itaanza kutekelezwa kikamilifu katika jimbo la Jamu na Kashmir, suala linalohitimisha sheria ya hali makhsusi katika eneo hilo.
Mabadiliko hayo tayari yamepasishwa na Rais wa India.
Hatua hiyo pia itafuta marufuku inayowazuia watu kutoka nje ya Kashmir kununua milki katika eneo la Jamu na Kashmir.
Mipango kama hii iliyochukuliwa hapa awali na serikali ya India ilikabiliwa na jibu kali la wakazi wa eneo la Kashmir na kusababisha machafuko makubwa. Viongozi wa vyama vya siasa wa Kashmir pia wametahadharisha kuhusu hatua ya kufutwa sheria ya hali makhsusi ya eneo hilo na kusisitiza kuwa, hatua hiyo itasababisha machafuko makubwa.   
Baada ya kutangazwa hatua hiyo India imezisha hatua kali za usalama katika eneo la Kashmiri ikiwa ni pamoja na kukata huduma za mwasiliano ya simu na intaneti.
parstoday.

Comments