Askari usalama wa Nigeria jana Jumatatu waliwatawanya washiriki wa maandamano yaliyopewa jina la "Mapinduzi Sasa" katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lagos.
Imeripotiwa kuwa, watu zaidi ya kumi wakiwemo waandishi habari wawili wanaofanya kazi katika mtandao wa habari wa Sahara wametiwa mbaroni katika maandamano hayo.
Askari usalama mjini Lagos wameuweka chini ya udhibiti mtandao huo wa habari na wanaendelea kuuchunguza.
Waandamanaji hao walikabiliana na askari usalama ambao walitumia gesi ya kutoa macho kuwatawanya.
Maandamano ya "Mapinduzi Sasa" yanafanyika nchi nzima dhidi ya serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria iliyoingia madarakani kwa kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Februari mwaka huu.
Juzi Jumapili polisi ya Nigeria ilitoa taarifa ikitahadharisha kuwa maandamano yaliyopangwa kufanyika jana kuwa ni kosa la uhaini.
Omoyele Sowore ambaye ni mchapishaji wa mtandao wa Sahara ambaye aligombea kiti cha urais kupitia chama cha African Action Congress mwezi Februari mwaka huu ameyataja maandamano hayo kuwa yanapinga uongozi mbaya wa serikali ya Abuja.
Sowore alikamatwa Jumamosi iliyopita akiwa nyumbani kwake.
parstoday.
Comments