
Akizungumza na Kamati ya maandalizi ya sherehe za Jamboree, katika ukumbi wa Wizara hiyo Mazizini Mjini Unguja amesema Wizara ya Elimu ndio msimamizi Mkuu wa sherehe hizo hivyo ni vyema kuzidisha mashirikiano kati ya Wizara, mashirika na taasisi nyengine ili kufikia malengo.
Aidha Mhe Riziki ambae pia ni Makamo Rais wa Chama Cha Skauti amesema sherehe hizo zitasaidia kuwapa uelewa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa kwa kuwa wakakamavu, wazalendo na wenye upendo na nchi yao.
Nae Mkuu wa Skauti Tanzania Bi Mwantumu Bakari Mahiza amesema lengo la kufanya sherehe hizo ni kuwajenga Vijana wawe na umoja na mshikamano, upendo na uzalendo wa kweli kwa nchi zao.
Hata hivyo ameitaka kamati ya maandalizi ya sherehe za Jamboree, kupata ushiriki kutoka Tamisemi pamoja na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknologia za Serikali ya Muungani Tanzania kutokana na kuwa kila kinachofanyika waweze kukitambua kwa Vijana wao kutokana na umuhimu wake.
Pia ameomba kufanya bidii ya kuwaandaa Vijana kutokana na kuwepo tatizo la upatikanaji wa fedha katika kuendesha shughuli zao kwani wanashindwa kufanya vizuri hasa katika suala zima la maandalizi ya sherehe hiyo, hivyo ni vyema kuwasaidia Vijana hao ili kuweza kuendeleza Skauti Tanzania.
Nae Mkurugenzi wa Idara ya Michezo na Utamaduni wa Wizara ya Elimu Bwana Hassan Tawakal Khairalla amesema katika kufikia sherehe hizo jumla ya maeneo 14 yataguswa ikiwemo kutembelea maeneo ya kihistori, kushiriki kazi maalum, pamoja na kushiriki katika utoaji wa taaluma mbalimbali ikiwemo namna ya kujikinga na majanga.
Sherehe za skauti ambazo zimepewa jina la "Jamboree" hufanyika kila mwaka ambapo kwa mwaka huu zitafanyika Zanzibar kuanzia tarehe 24 na kumalizika tarehe 28 Juni ikiwa Mikoa sita ya pwani inatarajiwa kutoa washiriki 24 kwa kila mkoa, pamoja na wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki.





Comments