Mchumba wa Jamal Khashoggi, mwandishi habari mkosoaji wa utawala wa Aal-Saud aliyeuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki mwaka jana ameitaka Marekani kuanzisha uchunguzi wa mauaji ya kutisha ya mpenzi wake huyo ambaye alikuwa amepanga kufunga naye ndoa kabla ya kuuawa.
Hatice Cengiz alitoa mwito huo jana Alkhamisi alipofika mbele ya kamati ya Kongresi ya Marekani mjini Washington, ambapo sambamba na kukosoa kimya cha jamii ya kimataifa kwa mauaji hayo, ameitaka serikali ya Marekani ianzishe uchunguzi na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa ukatili huo.
Cengiz ameeleza bayana kuwa, "Sio Jamal Khashoggi tu aliyeuawa, bali pia thamani za Marekani." Utawala wa Rais Donald Trump umekuwa ukikosolewa na mashirika ya kutetea haki za binadamu dunia kwa mienendo yake hasi ya kuukingia kifua utawala wa Riyadh ambao ulikiri kutekeleza unyama huo.
Hii ni katika hali ambayo, mwezi uliopita wa Aprili, gazeti la Washington Post la nchini Marekani lilifichua kuwa, genge la mauaji la Saudi Arabia lililomuua kikatili mwandishi huyo mkosoaji, Jamal Khashoggi walipata mafunzo nchini Marekani.
Tarehe pili Oktoba mwaka jana 2018, maafisa 15 wa serikali ya Saudi Arabia walitumwa mjini Istanbul Uturuki wakitokea Riyadh kwenda kumuua mwandishi huyo wa habari aliyekuwa anaukosoa utawala wa hivi sasa wa Saudia.
Serikali ya Saudi Arabia awali ilikanusha kuhusika na mauaji hayo, lakini baada ya mashinikizo kuwa makubwa ililazimika kukiri kuwa timu ya mauaji iliyomuua kinyama Jamal Khashoggi ilitumwa na serikali kwenda kumsaili mwandishi huyo na kwamba eti aliuawa kimakosa katika usaili huo.
parstoday.
Comments