Kuongezeka mvutano kati ya Imarati na serikali iliyojiuzulu ya Yemen.

Kuongezeka mvutano kati ya Imarati na serikali iliyojiuzulu ya Yemen
Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati, ambayo iko katika muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia katika vita vyake vya kivamizi dhidi ya Yemen, imeingia katika mvutano mkubwa kati yake na serikali iliyojiuzulu ya Yemen ambayo hivi sasa ingali inadhibiti eneo la kusini mwa nchi hiyo.


Tofauti zilizoongezeka kati ya pande mbili hizo hazihusiani tu na miezi ya hivi karibuni bali zilianza kudhihiri mwaka 2017 na kuendelea kuongezeka taratibu tokea hapo. 
Hii ni katika hali ambayo Saudi Arabia nayo inahitiliafiana na Imarati hiyo hiyo kuhusiana na maeneo mengine ya kusini mwa Yemen. 
Hitilafu hizo zinahusiana na udhibiti wa maeneo hayo na watu wanaoishi huko. Imarati inafanya juhudi za kudhibiti maeneo mengi zaidi kusini mwa Yemen. 
Hivyo hitilafu zilizopo kati ya nchi mbili hizo zinahusiana na mashindano ya kudhibiti na kueneza ushawishi wao katika maeneo hayo. Katika kipindi hiki chote Imarati imekuwa ikifanya juhudi kubwa za kudhibiti kisiwa cha Socotra, milki ya Yemen.
Inaripotiwa kwamba imewapa mafunzo ya kijeshi askari 300 katika mji wa Aden na kutuma 100 kati yao katika kisiwa hicho, hatua ambayo imeongeza mvutano kati yake na serikali iliyojiuzulu ya Yemen inayoongozwa na Abdrabbuh Mansur Hadi. 
Serikali hiyo inaamini kuwa askari hao waliotumwa na  Imarati katika kisiwa cha Socotra ni miongoni mwa watu wanaopigania kujitenga eneo la kusini mwa Yemen na kusema kuwa ushirikiano uliokuwepo kati ya serikali hiyo na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia ulikusudia kupambana na harakati ya Ansarullah ya Yemen, ushirikiano ambao sasa umedhoofika na kutoweka.
Ahmed al-Maisiry, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Yemen amekosoa vikali hatua ya Imarati kutuma askari hao huko Socotra na kusema: 'Ushirikiano wetu na muungano huu wa kijeshi haukuwa na lengo la kuzishirikisha nchi hizo katika uendeshaji wa mikoa ya Yemen.'
Sababu nyingine ya kujitokeza hitilafu kati ya serikali iliyojiuzulu ya Yemen na Imarati ni uamuzi wa nchi hiyo wa kushirikiana kwa karibu na Wayemen wanaotaka kujitenga eneo la kusini mwa Yemen, na kupunguza ushirikiano wake na serikali hiyo ya Abdrabbuh Mansur Hadi. 
Ni kutokana na ukweli huo ndipo askari watiifu kwa serikali ya Mansur Hadi wakapigana kwa muda na wabeba silaha wanoungwa mkono na Imarati mnamo mwezi Aprili mwaka 2017. 
Kufuatia hali hiyo, Mansur Hadi alimuuzulu Aidarus az-Zubeidi, mkuu wa wakati huo wa mkoa wa Aden lakini muda mfupi baadaye akaunda Baraza la Mpito la Kusini kwa uungaji mkono wa Imarati. 
Kufutia hatua hiyo kimsingi mambo ya mji wa Aden yamekuwa yakiendeshwa na serikali mbili moja ikiwa ni hiyo inayoongozwa na az-Zubeidi kwa uungaji mkono wa Imarati na nyingine inaongozwa na Abdrabbuh Mansur hadi anayeungwa mkono na Saudi Arabia.
Wakati huohuo mwaka uliopita idadi kadhaa ya mahatibu, maimamu wa swala ya Ijumaa, viongozi wa makundi ya kisiasa na makamanda wa kijeshi waliuawa kigaidi katika eneo hilo la kusini mwa Yemen na hivyo kuvuruga kabisa usalama wa eneo hilo. 
Hali hiyo ilipelekea serikali iliyojiuzulu ya Mansur Hadi kuilaumu Imarati kuwa ndiyo iliyokuwa ikichochea mauaji hayo ya kigaidi kwa lengo la kuharibu usalama wa Aden na wa mikoa mingine ya kusini mwa Yemen inayodhibitiwa na serikali hiyo.
Kwa ujumla hali inayotawala katika maeneo ya kusini mwa Yemen inathibitisha wazi kwamba Imarati inafanya juhudi za kueneza ushawishi wake katika maeneo hayo na wakati huo huo kudhoofisha nafasi ya serikali iliyojiuzulu ya Mansur Kadi katika maeneo hayo. 
Hivyo tunaweza kusema kwamba mvutano uliopo hivi sasa kati ya pande mbili hizo utaendelea kuongezeka katika siku zijazo.
parstoday.

Comments