Tunu ahimiza watoto wa kike wawezeshwe kielimu.

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Zanzibar, Tunu Juma Kondo amewataka watoto wa kike kuchangamkia fursa ya elimu ili kupata wasomi wanawake wenye sifa za kuwa viongozi bora wa baadae.
Naibu huyo alieleza hayo katika muendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa kamati tekelezaji ya UWT wilaya ya Kaskazini ‘A’ huko Gamba Mkoa wa Kaskazini ambapo alisema elimu ndio nyenzo pekee itakayomkomboa mtoto wa kike.
Alieleza kwamba kwa sasa watoto wa kike wanatakiwa kujengewa mazingira rafiki ya kupewa elimu itakayowasaidia katika ujenzi wa maisha yao ya baadae.
Alisema wanawake wanaopewa fursa za uongozi, utendaji na utaalamu wa fani mbali mbali katika jamii wamekuwa mfano wa kuigwa katika utendaji na uchapakazi, hivyo hicho ni kipimo sahihi cha uadilifu uliotukuka kwa kundi hilo.
Alisema kwamba matarajio ya UWT ni kuona wanawake wanajitokeza kwa wingi kushindana na wanaume katika kuwania nafasi mbali mbali za uongozi katika chaguzi za kisiasa zijazo kwani wanawake wengi wana sifa za kiutendaji.
Alisema kila mwanamke anatakiwa kuchukua hatua ya kuwalinda na kuwasimamia watoto wa kike dhidi ya vitendo vya udhalilishwaji ili waweze kutimiza malengo yao.
Akizungumzia lengo la ziara hiyo, Tunu alisema ni kuwashukuru akina mama walioshiriki kumuombea dua na kumuunga mkono kwa kumuona anafaa kuongoza nafasi hiyo na hatimaye akateuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo.
Alieleza kwamba atakuwa kiongozi na mtendaji mchapakazi anayetekeleza majukumu yake kwa ushirikiano na kushauriana na watu anaowaongoza ili kufikia malengo mahsusi ya jumuiya hiyo.
Alisema ni lazima viongozi na watendaji wa Umoja huo wafanye kazi kwa bidii ili kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya ibara ya tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo Jipya la mwaka 2017 inayoeleza namna CCM inavyotakiwa kushinda kwa kishindo kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa kuongoza dola.
Aliwataka akina mama hao kulipa ada kwa wakati ndani ya umoja huo na CCM kwa ujumla ili kulinda haki zao za kuwa wanachama hai na wenye sifa za kuchagua na kuchaguliwa.
Aidha alisisitiza kuwa chama, jumuiya na serikali zitaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kuwaletea maendeleo endelevu wananchi ambao ndio wenye maamuzi ya kukiweka madarakani CCM.
Katika risasa yao UWT wilaya hiyo walisema kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaongeza wanachama wapya wa chama na Umoja huo ili kuongeza jeshi la kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Zanzibarleo.

Comments